Maafa ya virusi vya corona nchini India yameongezeka leo huku idadi yake ya kila siku ya vifo ikipindukia 3,600, huku zaidi ya nchi 40 zikituma msaada wa dharura wa matibabu kuisaidia nchi hiyo kupambana na mgogoro huo unaozidi kuwa mbaya. 

Marekani na mataifa kadhaa ya Ulaya yameanza kulegeza vizuizi wiki hii wakati kampeni za utoaji chanjo zikishika kasi, lakini janga hilo linaendelea kuwa baya zaidi katika maeneo mengi ya dunia. 

Siku ya juzi India iliripoti vifo 3,645 vilivyotokea katika saa 24 zilizopita, wakati visa vipya vilivyothibitishwa vikifikia rekodi mpya ya dunia ya zaidi ya 379,000. 

Janga la corona limesababisha vifo vya watu milioni 3.1 kote duniani, huku India ikiwa na zaidi ya vifo 200,000. 

Waziri wa afya wa India, Harsh Vardhan Shringla amesema nchi zaidi ya 40 zinatuma vifaa muhimu vya matibabu na hasa mashine za kusaidia kupumua na mitungi ya oksijeni.