Na. Saidina Msangi na Peter Haule, WFM, Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwingulu Nchemba, ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kutumia weledi na kuzingatia sheria katika kukadiria kodi kwa wafanyabiashara ili kulinda walipa kodi na kutanua wigo wa walipa kodi.

Dkt. Nchemba alitoa maagizo hayo Jijini Dodoma alipokutana na wakuu wa Idara na Taasisi za wizara hiyo, katika kikao kazi kilicholenga kutekeleza maelekezo yaliyotolewa hivi karibuni na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo aliiagiza Wizara hiyo kutatua changamoto za wafanyabiashara nchini kuhusu masuala ya kodi.

“Maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni muhimu yatekelezwe ipasavyo ili kulinda na kukuza uchumi wa nchi kwa kutoza kodi kwa staha, weledi na kwa mujibu wa Sheria na turekebishe mahali tulipoharibu”alisisitiza Dkt. Nchemba.

Aliitaka TRA kuacha kudai taarifa za miaka mingi ya nyuma ambayo iko nje ya sheria kwa wafanyabiashara ambazo zilikwishafanyiwa kazi,  kwani utunzaji wa kumbukumbu ni changamoto kwa wengi hivyo ni vema kuzingatia sheria na taratibu za namna ya kufanya ukadiriaji wa kodi.

“TRA nawataka mpeleke ujumbe makini kwa wafanyakazi wa TRA nchini nzima kwamba Serikali haijasema msikusanye kodi au mpunguze jitihada za kukusanya kodi hizo bali kinachoongelewa na kusisitizwa ni kukadiria na kukusanya kodi kwa kuzingatia sheria na taratibu, bila kuonea watu”alisisitiza Dkt. Nchemba

Aliongeza kuwa ili kuendelea kupata mapato ya kutosha nchini ni lazima kuwalea wafanyabiashara ili kuwajengea uwezo wa kiuchumi akitolea mfano wa ngoómbe wa maziwa anayetakiwa kupewa huduma muhimu kabla ya kumkamua maziwa.

“Mheshimiwa Rais alielezea changamoto ya Kushika akaunti, fedha za wafanyabashara, tuache vitendo hivyo, hapa hakuna mjadala ni lazima yafuatwe na sisi Wizara tutaendelea kufuatilia maelekezo hayo” alisema Dkt. Nchemba.

Alisisitiza Mamlaka ya Mapato Tanzania kuzingatia maelekezo aliyotoa na  kurekebisha pale ambapo sheria hazikuzingatiwa ili kulinda uchumi wa nchi na kutodhoofisha biashara za walipakodi pamoja na kuangalia namna ya kuongeza walipa kodi wapya.

Kwa upande mwingine Waziri Dkt. Nchemba ametoa rai kwa Watanzania wakiwemo wafanyabiashara kulipa kodi inavyostahili kwa kufuata Sheria na taratibu zilizopo na kuzingatia matumizi bora ya kutunza kumbukumbu za malipo.

Alieleza kuwa utamaduni wa kulipa kodi uwe jambo la kawaida na la kila siku kwenye maisha yetu, ujanja ujanja wa kukwepa kodi ni kuvunja sheria na Serikali haitavumilia.

Aidha amewataka wafanyabiashara walioziondoa fedha zao kwenye benki wazirejeshe na kuzihifadhi kwenye benki hizo na kuahidi kuwa zitakuwa salama na hazitazuiwa na TRA kwa kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kwa taasisi hiyo ili kurejesha ari ya ufanyaji biashara nchini.

Naye Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Masauni, alisema kuwa kikao kazi hicho kitawawezesha kujua hatua gani imefikiwa na Wizara ili kusimamia na kuendeleza uchumi wa nchi na Maisha ya watu.

Alisema kuwa ameona timu nzuri ya wataalam ndani ya Wizara ya Fedha na Mipango ambayo itasaidia kutimiza malengo ya Serikali, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na maelekezo yaliyotolewa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, hivi karibuni.

Mwisho