Ripoti ya uchunguzi ambayo imechapishwa leo imeonyesha kwamba vifo visivyopungua 1,150 ambavyo vimehusishwa na ugonjwa wa COVID-19 nchini India, havijajumuishwa kwenye takwimu rasmi za vifo, ishara kwamba huenda idadi ya vifo kutokana na janga hilo nchini India ni juu zaidi.

Uchunguzi huru uliofanywa na kituo cha utangazaji NDTV umebaini kuwa mamia ya vifo vinavyohusishwa na virusi vya corona havikujumuishwa kwenye takwimu rasmi ya serikali.

Picha zilizopigwa kutoka angani kuonyesha miili ikichomwa moto kulingana na tamaduni za maziko ya Wahindi, zimezusha mashaka kuhusu takwimu za serikali na hali halisi kuhusiana na idadi ya vifo.

Data zilizokusanywana manispaa ya mji huo kutoka kwenye vituo 26 vya kuchomea maiti zimeonyesha miili 3,096 ilichomwa kati ya Aprili 18 na Aprili 24. 

Lakini katika kipindi sawa na hicho serikali ya India ilirekodi vifo 1,938 tu. Sababu ya tofauti za data hizo haijajulikana. Vituo vipya vya kuchoma maiti vinajengwa mjini New Delhi mnamo wakati maambukizi na idadi ya vifo ikiongezeka.