Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) imeeleza kuwa Sh140 milioni ambazo Wizara ya Maliasili na Utalii iliilipa kampuni ya Wasafi hazikuwa na mkataba wowote uliosainiwa.

Wizara hiyo ililipa fedha hizo kwa ajili ya wasanii ambao wangetangaza utalii wa ndani katika mikoa sita nchini Tanzania.

Akizungumza leo Alhamisi Aprili 8, 2021 katika mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma CAG, Charles Kichere amesema, “Wizara ililipa Sh140 milioni kwa kampuni ya Wasafi kwaajili ya wasanii ambao wangetangaza utalii wa ndani katika mikoa sita, hata hivyo hakukuwa na mkataba wowote uliosainiwa baina ya wizara na kampuni ya Wasafi na kushindwa kuhakiki wigo na huduma iliyotolewa na kampuni ya Wasafi.”

Amesema kiasi hicho cha fedha kilicholipwa kwa Wasafi hakiendani na sheria za matumizi ya fedha za umma.

“Kamati iliyoundwa kwa ajili ya utekelezaji wa Tamasha la Urithi liliidhinisha bajeti ya sh Bilioni 1.6 hata hivyo bajeti hiyo haikuwasilishwa kwangu kwa ajili ya ukaguzi, kupitia ukaguzi wangu nilibaini pia kutokuwepo kwa mpango wa utekelezaji wa tamasha hilo.

Amebainisha upungufu uliobainika katika uanzishwaji wa tamasha la Urithi haukuwa na nyaraka zilizowasilishwa kwa ajili ya ukaguzi kuhusu matumizi hayo pamoja na Sh487 milioni zilipelekwa kwenye taasisi saba na kwamba hakukuwa na nyaraka zilizowasilishwa kudhibitisha matumizi hayo.

“Matumizi ya Sh585 milioni yaliyolipwa na mhasibu wa mfuko wa tozo ya maendeleo ya utalii hayakuwa na nyaraka toshelezi na kushindwa kudhibitisha uhalali wa malipo hayo,” amesema.