Aliyewahi kuwa Mbunge wa Singida Kaskazini na Waziri katika Serikali ya awamu ya Nne, Lazaro Nyalandu ametangaza kurejea katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) akitokea chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Ametangaza uamuzi wake huo leo mbele ya mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano mkuu maalum wa cCCM  uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma.

Waziri huyo wa zamani wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya awamu ya nne alijitoa CCM Oktoba 30, 2017 na baadaye alijiunga Chadema ambako alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Kati.

Nyalandu pia alijitosa ndani ya Chadema kuomba ridhaa ya chama hicho kumpitisha kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2021, hata hivyo aliangushwa na Tundu Lissu.

"Nimerudi  CCM,” alisema Nyalandu katika mkutano huu maalum wa CCM nakushukuru kwa kukubali kupokelewa.

“Hakika mwenyekiti hakuna furaha kama ya mtoto kusamehewa na kurejea nyumbani na haulizwi tena kuwa nyumbani unarudi lini.”

Akinukuu mstari wa Biblia katika kitabu cha Zaburi ya 137 mstari wa 1- 4 Lazaro alisema “Kando ya mito ya Babeli, ndipo tulipoketi, tukawa tunalia tulipoikumbuka Siyuni, katika miti ya nchi ile, tulitundika vinubi vyetu,waliotuteka walitutaka tuwaimbie; watesi wetu walitutaka tuwafurahishe: Tuimbieni mojawapo ya nyimbo za Sayuni!” Twawezaje kuimba wimbo wa Mwenyezi-Mungu katika nchi ya kigeni?”.

Lazaro aliongeza kwa kusema “Ugenini nyimbo haziimbiki, Mzee Lowassa (Edward) sijui kama yupo hapa, Mzee Sumaye (Fredrick) namuona hapa, Mzee wangu Wilbroad Silaha, hawa ni mashahidi kuwa nyimbo ya furaha haimbiki ugenini.

Alisema Watanzania wameiona nyota ya Rais Samia, wameguswa na kujawa na furaha na matumaini kwake kwa kuwa Mungu alimuandaa na kumuinua hivyo ni maombi ya watanzania wote kuwa mkono wa Mungu ukamuongoze aweze kutekeleza yote aliyoahidi.

 “Mama Neno lako likaponye wale wote waliumia, mama ukaitwe heri wa mioyo ya watanzania, ukaongeze tabasamu katika nyuso za watanzania wote kwa kuendeleza matamanio yao juu ya taifa lao, uliongoze  kwa misingi hiyo hiyo aliyoasisi Mwalimu Julias Nyeree ya Uhuru, Haki, Umoja na Mshikamano.” alimalizia kwa kusema .