Serikali imeagiza kuvunjwa kwa bodi ya manunuzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kutokana na kutoridhishwa na utendaji kazi wake.

Agizo hilo limetolewa jijini Dodoma na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani,wakati akifunga mkutano uliowakutanisha Watendaji wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) pamoja na Wahandisi na Mameneja wa TANESCO wa mikoa mbalimbali nchini kwa lengo kutathmini utekelezaji wa miradi ya usambazaji nishati vijijini.

Dkt. Kalemani amesema bodi hiyo ya manunuzi ya TANESCO imekuwa ikilalamikiwa kutokana na ukiritimba uliopo katika suala la manunuzi, kwa kukiuka kanuni.

“Lazima bodi hii ivunjwe kuanzia leo hii na ichaguliwe nyingine na ianze kazi leo hii, maana yake kumekuwa na ukiritimba mkubwa sana katika manunuzi, anaachwa mtu mwenye bei ndogo katika manunuzi na kuchukuliwa mtu mwenye bei juu hii sio sawa.” amesema Dkt. Kalemani.

Mbali na kuvunjwa kwa bodi hiyo ya Manunuzi ya TANESCO, Waziri Kalemani  ameagiza uchunguzi ufanyike kwa wahusika wote waliokuwa wakilalamikiwa juu ya ukiukwaji wa sheria za manunuzi na wachukuliwe hatua za kisheria.

Dkt. Kalemani amewaagiza  Mameneja wote wa TANESCO nchini, kuhakikisha wanaongeza kasi ya usambazaji wa umeme katika maeneo yaliyosalia.

“Azma ya Serikali ni huduma hii ya umeme kufikia vijiji vyote vilivyosalia ifikapo Desemba 2022, hivyo kuanzia sasa tuna miezi 18 kukamilisha zoezi hili ili kuvifikia vijiji vyote vilivyobaki, na ambaye hatafikia lengo hatavumilika kabisa,” amesema Waziri Kalemani.

Aidha Dkt. Kalemani amepiga marufuku mgao wa umeme na ukataji wa umeme bila kutoa taarifa kwa Wananchi, na kuonya kuwa atakayeshindwa kutimiza jambo hilo atapoteza nafasi yake.