Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza jana hatua sita za rais ambazo serikali yake itazichukua katika juhudi za kukabiliana na kile alichokiita janga la mashambulizi ya silaha yaliyoligubika taifa hilo.

Biden ameyaita mashambulizi ya silaha kuwa ni mzozo wa kiafya wa kitaifa unaoigharimu Marekani, sio tu kimaisha na mustakabali wa raia wake, lakini pia kiasi kinachokadiriwa kufikia dola bilioni 280 kila mwaka.

Amesema, kwenye mkutano na waandishi wa habari nje ya ikulu ya White House kwamba ni lazima mashambulizi hayo yafikie mwisho. 

Miongoni mwa hatua ambazo atazisaini mara moja ni pamoja na kuwataka watu wanaonunua vifaa na kuunda silaha nyumbani kuchunguzwa kwanza historia zao, ama wale wanaotaka kuzifanya silaha zao kuwa kali zaidi kuwasilisha majina kwenye mamlaka kabla ya kuruhusiwa kununua vifaa hivyo.

Makamu wa rais Kamala Harris na mwanasheria mkuu Merrick Garland pia walihudhuria tukio hilo.