Rais Joe Biden ameahidi kupunguza kwa nusu viwango vya utoaji wa gesi ya ukaa nchini Marekani, kufikia mwishoni mwa muongo huu, wakati akifungua mkutano wa kilele wa mtandaoni uliohudhuriwa na viongozi 40 wa dunia kuhusu mabadiliko ya tabianchi. 

"Tunajua umuhimu wa hili, kwa sababu wanasayansi wanatuambia kwamba huu ni muongo wa maamuzi. Huu ndiyo muongo ambamo tunapaswa kufanya maamuzi yatakayoepusha madhara mabaya zaidi ya mzozo wa tabianchi," alisema Biden. 

Mkutano huo wa siku mbili unalenga kuyahamasisha mataifa yenye uchumi mkubwa kuweka malengo makubwa zaidi ya kupunguza viwango vya gesi ya kaboni, na unatazamwa kama maandalizi muhimu kuelekea mkutano wa mazingira wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika mjini Glasgow, Scotland, mwezi Novemba.