Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Urusi Alexei Navalny amehamishwa na kupelekwa kwenye hospitali ya wafungwa siku ya 20 tangu alipoanza mgomo wa kula. 

Afisa wa huduma za magereza pamoja na wakili wake wamesema hayo katika wakati shinikizo la kimataifa linaongezeka dhidi ya Urusi kufuatia wasiwasi kuwa mwanasiasa huyo huenda angefariki akiwa jela.

Idara ya huduma za magereza imesema uamuzi wa ulifikiwa wa kumhamisha Navalny mwenye umri wa miaka 44 hadi katika hospitali inayowahudumia wafungwa, na kwamba hali yake ya afya ilikuwa ya ‘kuridhisha’.

Washirika wa Navalny ambao walishindwa kumfikia tangu wiki iliyopita, walisema wanahofia afya yake. Wamepanga maandamano makubwa kote nchini Urusi Jumatano wiki hii, maandamano ambayo mamlaka za Urusi zimetaja kuwa kinyume cha sheria.

Masaibu ya Navalny yameitenga Urusi zaidi mnamo wakati utawala wa rais wa Marekani Joe Biden umetangaza vikwazo zaidi vya kiuchumi, nayo Jamhuri ya Czech ambayo ni mwanachama wa NATO na pia wa Umoja wa Ulaya ikiwa imewafukuza makachero wa Urusi ikiwatuhumu kuhusika na shambulizi hatari la mwaka 2014 kwenye ghala lao la silaha.