Vyombo vya habari nchini Myanmar vimesema watu kadhaa wameuawa jana Jumamosi ikiwa ni tukio baya zaidi kutokea tangu mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika mwezi uliopita. 

Zaidi ya watu 70 wameuawa wakati vikosi vya usalama vilipowafyatulia risasi waandamanaji wanaotetea demokrasia. 

Jamii ya kimataifa imelaani mauaji hayo huku balozi za Jumuiya ya Ulaya pamoja na Uingereza zikielezea kusikitishwa na mauaji ya raia wakiwemo watoto ambayo yamefanyika sanjari na maadhimisho ya 76 ya Siku ya Vikosi vya jeshi nchni Myanmar. 

Ujumbe wa Umoja wa Ulaya uliopo nchini Myanmar umesema siku hii itabaki kwenye kumbukumbu za watu kama ni siku ya vitendo visivyoweza kusahaulika vya ugaidi na fedheha kwa raia wa Myanmar. 

Mabalozi wa Umoja wa Ulaya na Uingereza nchini Myanmar wamesema jeshi limezidi kujivunjia hadhi yake kwa kuwapiga risasi raia ambao hawakujihami. Ukatili dhidi ya wapinzani unaendelea nchini humo hata baada ya watawala wa kijeshi kusema watawalinda watu na kujitahidi kuitetea demokrasia.