Waziri Ummy Awaahidi Wanawake Kuanzisha Dirisha Maalum NEMC La Kusaidia Biashara Na Uwekezaji Wa Wanawake
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Ummy Mwalimu amewaahidi Wanawake kuwasaidia kuanzisha dirisha maalumu la kuwasaidia katika uwekezaji ili kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili wanapotaka kuwekeza, amesema atahakikisha anatoa kipaumbele kwenye kutoa vibali vya Mazingira ili mradi tu biashara au uwekezaji unafanywa na mwanamke.
Ameyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji Tuzo za Viwanda kwa Wanawake Wajasiriamali Tanzania iliyoandaliwa na Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (Tanzania Women Chamber of Commerce) kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
“Nawa ahidi kupitia NEMC nitaanzisha dirisha maalum la biashara na uwekezaji ili kuweka mazingira mazuri kwa mwanamke anayetaka kuwekeza awekeze bila vikwazo, moja ya kipaumbele ni kuhusu vibali kutoka kwa wakati” alisema Waziri Ummy.
Mhe. Ummy ameongeza kuwa mwanamke asiwe mtu wa kukata tamaa, ajitume na kuondoa uoga kwamba jamii itamchukulia kwa mtazamo tofauti atakapowekeza au kufanya biashara fulani. Hii itamsaidia kufikia malengo aliyojiwekea yatimie kwa mafanikio makubwa.
“Ndugu zetu wanaume hawaogopi ndiyo maana wapo mbali katika kufanya biashara na uwekezaji kwahiyo nasisitiza kuwa mwanamke aondoe hofu anapotaka kuwekeza, afanye kazi kwa bidii ili aweze kufikia malengo na mafanikio makubwa katika uwekezaji” Mhe. Ummy alisema.
Mhe. Ummy amewaomba wanawake washirikiane, wasaidiane wawe na umoja linapokuja suala la biashara na uwekezaji kwa wanawake.
“Nimeona kuna majukwaa mengi ya wanawake yanayohusu biashara na uwekezaji, lakini ningependa liwepo jukwaa moja la biashara, viwanda na uwekezaji linalowaunganisha wanawake.”
Aidha Mhe. Ummy ametoa rai kwa wanawake kuchangamkia fursa kwenye sekta ya mazingira, mfano kupitia marufuku ya mifuko ya plastiki watengeneze mifuko mbadala. Pia watumie nishati mbadala wakati wa uzalishaji kuliko kutumia nishati ya miti, hii itasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira na kuzuia mabadiliko ya tabianchi.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Watoto, Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Bi. Mwajuma Magwiza, amesema kupitia mamlaka za Serikali za Mitaa, Serikali imekuwa ikitenga fedha za mikopo yenye masharti nafuu kwa wanawake kupitia vikundi ili kuwapa fursa ya kuanzisha biashara na uwekezaji.
Akiongea katika hafla hiyo, Rais wa wanawake wajasiriamali Tanzania Bi Maida Waziri, amesema adui wa mwanamke siyo mwanamke bali ni umasikini, wanawake washirikiane kuukataa umasikini kwa vitendo kupitia upendo, kusaidiana na kushirikiana katika biashara na uwekezaji kwenye vyama vyote vya wanawake ili viwe na nguvu katika kutatua matatizo au changamoto zinazowakabili wanawake.
“Natoa rai kwa vyama vyote vya wanawake wajasiriamali viungane ili viwe na umoja wenye nguvu ya kuyasemea matatizo yao kwenye vyombo vya Serikali na kupatiwa ufumbuzi kwa urahisi.”