Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema alizuiwa kusafiri kwenda Umoja wa Falme za Kiarabu kupitia anga ya Saudi Arabia wiki iliyopita kutokana na kitisho cha kushambuliwa kwa kombora na waasi wa Iran walioko Yemen.

 Kauli hiyo imetolewa jana Jumamosi baada ya Netanyahu wiki iliyopita kuahirisha ziara yake kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu, kufuatia mzozo na jirani yake Jordan ambayo imefungia kwa muda ndege ya waziri mkuu huyo kutumia anga lake. 

Waziri mkuu huyo pia alishindwa kutumia anga ya Saudi Arabia akisema kulikuwa na changamoto wiki moja iliyopita, akikusudia shambulizi la kombora la hivi karibuni lililofanywa na waasi wa Houthi wa nchini Yemen. 

Hata hivyo Netanyahu hakutoa maelezo ya kina kuhusu matamshi hayo wala kueleza iwapo ndege yake ilikuwa ikilengwa na wanamgambo wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran.