Serikali imeridhishwa na kazi inayoendelea kufanywa na viongozi wa wizara ya kilimo na wataalam wake kuhakikisha makundi ya nzige yaliyovamia mikoa ya Manyara, Kilimanjaro na Arusha yanavyodhibitiwa kwa kuuwawa.


Kauli hiyo ya serikali imetolewa leo (04.03.2021) wilayani Monduli mkoa wa Arusha wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea kijiji cha Engaruka kukagua zoezi la kunyunyuzia viuatilifu kuua makundi ya nzige na kuwa amefurahi kuona kazi hiyo imefanyika kwa mafanikio chini ya uongozi wa Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda.


Waziri Mkuu aliyeambatana na Wakuu wa Mikoa wa Arusha, Manyara na Kilimanjaro alisema serikali inatambua na kuthamini kazi kubwa iliyofanywa na wataalam wa wizara ya Kilimo pamoja na wale wa halmashauri za Mwanga, Siha, Longido, Simanjiro na Monduli kuwadhibiti makundi ya nzige licha ya ugumu wa mazingira ya porini.


“Nimeridhika na kazi iliyofanyika hadi sasa kuwadhibiti nzige waliovamia maeneo ya mikoa yetu ya Manyara, Kilimanjaro na hapa Arusha. Wizara ya Kilimo imechukua hatua madhubuti, endeleeni kuhakikisha wadudu hawa hawasambai kwenye mikoa ya jirani “ alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.


Katika hatua nyingine Waziri Mkuu ameagiza wizara ya Kilimo kutenga fedha katika bajeti ya mwaka 2021/22 kwa ajili ya kufufua Kitengo Cha Kilimo Anga ili kitumike kwa ajili ya kudhibiti wadudu waharibifu wakiwemo nzige kwa kuwa na vifaa na wataalam wa kutosha.


Alibainisha kuwa kwa kuwa sasa ni msimu wa kilimo, hakuna budi kwa maafisa kilimo kwenye mikoa yote nchini wakawa na utaratibu wa kufuatilia kwa karibu uwepo wa viashiria vya nzige ili kuijulisha wizara kwenda kudhibiti mapema kabla hawajasambaa kwenye maeneo ya mashamba na kuzaliana.


“Hatuwezi kuwapa nafasi nzige wazaliane hapa nchini kwani watapoteza malisho yetu na mazao ya chakula pia biashara .Nzige kwetu ni adui hatari hatupaswi kuwapa nafasi hata dakika moja, hawa tuliwasikia kwa ndugu zetu Kenya na tulitoa ushirikiano kuwaangamiza lakini wamefika nchini lazima tuwaangamize wote” aliagiza Waziri Mkuu.


Akitoa taarifa ya kazi ya kudhibiti nzige Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda alimweleza Waziri Mkuu kuwa kundi la kwanza la nzige liliingia nchini mwezi Januari wilayani Mwanga na mwezi Februari kundi jingine liliingia wilaya ya Longido na kusambaa kwenye wilaya za Simanjiro, Siha na Monduli.


Prof Mkenda alisema tayari wizara kwa kushirikiana na mikoa hiyo iliyokumbwa imefanikiwa kuangamiza makundi ya nzige kwenye wilaya ya Mwanga na Siha.


“Longido tuliangamiza makundi ya nzige lakini kundi dogo likakimbilia Monduli hapa Engaruka na kazi ya kuangamiza imeanza tunakwenda vizuri, tuna hakika tutawamaliza wote kwani tunavyo vifaa kama mabomba ya kuliza kwa mikono, helkopta na ndege maalum zinafanya kazi “ alisema Prof. Mkenda.


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha Idd Kimanta alipongeza kazi inayofanywa na wizara ya kilimo kwa kuja eneo la tukio mapema ambapo Waziri na Naibu wake muda wote wamekuwa vijijini kushirikiana na wananchi kudhibiti makundi ya nzige.


Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alimweleza Waziri Mkuu kuwa vijiji vya Nondoto, Irelendeni na Engaruka wilaya ya Monduli ndipo makundi ya nzige yalipo kwa sasa na kuwa operesheni ya kuangamiza imefanyika jana na leo ha kuwa hali inaendea vema nzige wengi wamekufa.


Akihitimisha hotuba yake Waziri Mkuu aliwasihi wananchi kote ambako nzige wameonekana kutokuokota nzige waliokufa kwani wameuwawa kwa sumu inayoweza kuleta madhara kwa binadau endapo akila nzige hao.


Waziri Mkuu Majaliwa amehitimisha ziara yake ya siku moja wilayani Monduli kwa kuongea na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Engaruka ambapo amesema serikali ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli itakamilisha ujenzi wa barabara ya lami toka Mto wa Mbu hadi Engaruka Monduli .
Mwisho
Imeandaliwa na;
Kitengo cha Mawasilino Serikalini
Wizara ya Kilimo
MONDULI
04.03.2021