Na: Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ametatua kero na changamoto zilizokuwa zikiwakabili wafanyakazi wa Shamba la Mkonge la Kigombe Estate, Wilayani Muheza dhidi ya mwajiri wao kufuatia malalamiko ambayo yaliwasilishwa wakati wa ziara ya Waziri Mkuu.

Akizungumza wakati wa ziara yake hiyo ya kikazi ambayo ilikuwa imelenga utekelezaji wa Maagizo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliyoyatoa tarehe 21 Januari, 2021 alipotembelea shamba hilo la Mkonge lililopo chini ya kampuni ya Amboni Plantation Limited.

Mara baada ya kusikiliza pande zote mbili Waziri Mhagama alieleza kuwa kutokana na malalamiko mbalimbali yaliyowasilishwa na wafanyakazi inadhihirisha kuwepo na mapungufu makubwa katika utekelezaji wa sheria za kazi ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa migogoro kutokea.

“Mwajiri anawajibu wa kusikiliza kero na malalamiko ya wafanyakazi waliyonayo na kutafuta ufumbuzi kwa pamoja ili kutatua changamoto zinazowakabili wafanyakazi wake, mkifanya hivyo mtaongeza tija na ufanisi katika utendaji wa majukumu yenu,” alisema Wazir Mhagama.

Alieleza kuwa, wajibu wa mwajiri ni kufuata sheria na miongozo ya ajira mahala pa kazi ili kila mfanyakazi aweze kupata haki na utekelezaji wa masuala hayo utawawezesha kuwa na mahusiano mazuri kati ya mwajiri na watumishi alionao.

Aliongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli imekuwa mstari wa mbele katika kusimamia wanyonge na imekuwa ikiwasikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

“Kwetu sisi Mawaziri tumekuwa tukitekeleza hayo kwa kukutana na wananchi mbalimbali ikiwemo mimi Waziri ambaye nasimamia masuala ya kazi nipo hapa kwa ajili ya kutatua kero zenu na kutafuta ufumbuzi wa pamoja ili kujenga mazingira bora ya utekelezaji wa majukumu yetu mahala pa kazi,” alieleza

Sambamba na hayo, Waziri Mhagama alitoa maagizo ikiwemo kukitaka Chama cha Wafanyakazi wa Shamba la Mkonge la Kigombe Estate lililopo chini ya kampuni ya Amboni Plantation Limited kujenga tabia ya kukutana na mwajiri mara kwa mara kwa kuzingatia tija na uzalishaji wa kiwanda hicho na kushauriana namna ya kuongeza mishahara na posho kwa wafanyakazi wake.

Suala la pili, Maafisa Kazi kusimamia utekelezaji wa Sheria za Kazi katika Shamba la Mkonge la Kigombe Estate lililopo chini ya kampuni ya Amboni Plantation Limited, wilayani Muheza.

Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kusimamia michango ya wafanyakazi hao katika mfuko huo wa hifadhi ya jamii na kuendelea kutoa elimu kwa wafanyakazi kuhusu fao la upotevu wa ajira ili watambue sheria inawajibika pale mhusika ameachishwa kazi na siyo kuacha kwa hiyari.

Pia alitoa maagizo kwa Mamlaka ya Maji Safi kuhakikisha maji kupima maji yanayotumiwa na wafanyakazi hao ili waweze kupata maji safi na salama. Pia amewataka TRA pamoja na NIDA kushughulika kwa karibu suala la vitambulisho vya uraia ili TRA waweze kuwapatia TIN namba wafanyakazi ambao walisimamishwa kazi kurejea sehemu zao za kazi katika shamba hilo.

Sambamba na hayo Waziri Mhagama alimpongeza Mbunge wa jimbo hilo kwa kuwa karibu na wafanyakazi hao pamoja na kushirikiana na viongozi wa serikali katika kutatua kero zinazowakabili wafanyakazi hao wa Shamba la Mkonge la Kigombe Estate, lililopo Wilayani Muheza.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Muheza Mhe. Hamis Mwinjuma alieleza kuwa ziara hiyo ya Waziri itarejesha matumaini kwa wafanyakazi hao wa Shamba la Mkonge la Kigombe Estate kutokana na wataalam mbalimbali alioambatana nao hivyo malalamiko na kero mbalimbali za wafanyakazi hao zitapatiwa ufumbuzi.