Na Munir Shemweta, WANMM
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amemaliza utata uliojitokeza mtaa wa Nzasa kata ya Kijitonyama katika Manispaa ya Kinondoni Dar es Salaam baina ya baadhi ya wakazi wa mtaa huo na mmiliki wa viwanja  namba 296 na 297 Dkt Khalifa Mussa Msami kuhusiana na umiliki pamoja na mipaka ya eneo hilo.

Waziri Lukuvi alienda katika eneo hilo lililopo barabara ya Segera tarehe 15 Machi 2021 baada ya kupokea malalamiko kuhusiana na matumizi pamoja na mipaka ya eneo hilo.

Akiwa katika eneo hilo, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alibaini uliukwaji wa mipaka ya maeneo hayo huku  baadhi ya wamiliki katika nyumba za mtaa huo wakiongeza ukubwa wa maeneo yao na kuingia sehemu ya barabarani kwa takriban mita nne na wengine wakiziba mifereji ya maji taka.

Kufuatia hali hiyo, Waziri Lukuvi aliagiza ofisi ya ardhi mkoa wa Dar es Salaam pamoja na idara ya ardhi katika halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuhakikisha inafufua mipaka ya maeneo hayo haraka ili kubaini wamiliki waliojiongezea maeneo kinyume na sheria.

“Uamuzi wangu baada ya kubaini ukiukwaji, timu ya wilaya na mkoa ije ifufue mipaka bila kubomoa nyumba na mjue ni kosa kujiongezea eneo. Ukimilikishwa jenga kwa mpango wa serikali siyo kujiamulia na heshimu mipaka ya serikali ” alisema Lukuvi.

Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, timu kutoka ofisi hizo mbili itakapoenda kufufua mipaka katika eneo hilo  itamuonesha kila mmiliiki eneo lake ambapo alisisitiza kuwa, baada ya kukamilika kazi hiyo kila mmiliki wa ardhi atatakiwa kubaki eneo lake kulingana na ukubwa wa kiwanja chake na maeneo ya barabara pamoja na njia za maji taka yaachwe wazi.

“Lakini tushajua katika viwanja vyenu kuna walioongeza maeneo kwa madai kuwa ni maeneo ya wazi, msitamani vitu vya watu wengine ,mjenge kwa kuzingatia maeneo yanayowahusu na si vinginevyo. Alisema Waziri Lukuvi.

Baadhi ya wamiliki wa nyumba katika Mtaa huo wa Nazasa, kata ya Kijitonyama Manispaa ya Kinondoni walimueleza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa walifanya maamuzi hayo ya kuongeza maeneo bila kujua na kudhani maeneo hayo ni ya wazi na kumuomba Waziri Lukuvi kungalia namna ya kuwasaidia kwa kuwa wameshajenga katika maeneo hayo..