Na Munir Shemweta, WANMM
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe William Lukuvi amehitimisha mgogoro wa muda mrefu baina ya wananchi wa eneo la Chasimba, Chatembo na Chachui katika kata ya Bunju na Wazo Manispaa ya Kinondoni na Kiwanda cha Saruji cha Tanzania Portland (Wazo Hill) ambapo kiwanda hicho kimekubali kuachia hekta 224.8 kati ya 922.55 kwa wananchi wa eneo hilo.


Uamuzi wa wananchi kuachiwa hekta 224.8 unafuatia Serikali kuingilia kati mgogoro huo mwaka 2015 baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi na kuamua kutafuta suluhu kwa kuangalia namna bora ya kutekeleza uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kuhusiana na mgogoro huo.


Akizungumza na wananchi wa eneo hilo jijini Dar es Salaam tarehe 13 Machi 2021 alisema, Baada ya mazungumzo marefu na uongozi wa kiwanda ikiwemo bodi ya Kiwanda cha Saruji cha Wazo kilikubali kuachia eneo lake lenye thamani ya zaidi ya bilioni 60 kwa wananchi.


Waziri Lukuvi alisema, Serikali ya Awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli muelekeo wake ni kutetea wanyonge na shukurani kubwa apewe Mhe. Rais Magufuli kwa uamuzi kuwatetea wanyonge na kusisitiza kuwa, maamuzi ya kutovunja nyumba hayaingilii maamuzi ya Mahakama ya Rufaa bali yanalenga kunufaisha pande zote mbili.


Alieleza kuwa, kufuatia suluhu ya mgogoro huo sasa kila mwananchi katika eneo hilo atatakiwa kulipa gharama za kumiliki shilingi  6,400 kwa mita ya mraba ikiwa ni juhudi za serikali wakati wa majadiliano na kiwanda cha saruji ambapo hapo awali wamiliki walitaka wananchi walipe shilingi 20,000 kwa mita za mraba. Waziri Lukuvi aliongeza kuwa, baada ya kumalizika mgogoro huo sasa wananchi wa maeneo hayo wataanza kupatiwa ankara za malipo kujua kiasi wanachotakiwa kulipa katika maeneo yao yanayohusisha mitaa mitatu ya  Boko, Basiaya na Wazo.


“Eneo hili mlilovamia ninyi lina  mambo mawili, kwanza wenye eneo  wana hati za umiliki pamoja na leseni za madini na ninyi mmezuia kiwanda kisifanye kazi. Mimi nilinunua kesi na kufanya jambo hili kwa miaka mitano na nimetumia kila uwezo wangu na leo nahitimisha suala hili” Waziri Lukuvi.


Waziri Lukuvi limuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Sipora Liana na timu yake kwenda katika eneo hilo na kukagua maeneo yanayohitajika kwa ajili ya shughuli za huduma za jamii kama vile shule na zahanati ili kuanza ujenzi kwa kuwa wananchi wa maeneo hayo wanahitaji huduma hizo.


Aidha, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alipiga marufuku wananchi kuanza kuvamia tena maeneo ya kiwanda na kusisitiza kuwa,  hakutakuwa na huruma ya kuongeza mita za mraba katika eneo hilo kwa watakaovamia.


Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Daniel Chongolo alimshukuru Waziri Lukuvi kwa kusimamia na hatimaye kutatua mgogoro huo na kubainisha kuwa  kutokana na kazi kubwa inayofanywa na Wizara ya Ardhi kwa sasa migogoro ya ardhi kwenye wilaya yake imepungua sana ambapo hapo awali ilikuwa ikioongoza kwa asilimia  75.


Mkazi wa Chasimba Bi. Semeni Charles aliishukuru Serikali hasa Rais John Pombe Magufuli kwa kutetea wanyonge katika suala hilo na kueleza kuwa sasa wataishi kwa amani tofauti na hapo nyuma ambapo walikuwa hawajui hatma yao juu ya suala hilo.


Awali, wananchi wa eneo hilo wapatao 932 mwaka 2008 walifungua kesi Namba 129 katika Mahakama ya Rufaa Tanzania kuomba kutambuliwa kama wamiliki halali wa eneo hilo ambapo hata hivyo walishindwa kesi na kuamuriwa kubomolewa nyumba zao.


Kutokana na suluhu ya mgogoro huo eneo hilo limepatikana viwanja 4000 vya ukubwa na matumizi mbalimbali pamoja na maeneo ya barabara na huduma za jamii ambapo wananchi waliobakishwa katika eneo hilo sasa watatakiwa kulipa gharama za kumiliki kulingana na ukubwa wa eneo.


Eneo la Chasimba, Chatembo na Chachui katika kata za Bunju na Wazo jijini Dar es Salaam ambalo lilikuwa maarufu kwa uchimbaji wa chokaa na kokoto liliingia kwenye mgogoro mwaka 2008 kati ya wananchi wa eneo hilo na Kiwanda cha Saruji cha Tanzania Portland (Wazo Hill) kutokana na wananchi kuvamia eneo hilo ambapo baada ya kufanyika uhakiki ilibainika jumla ya hekta 224.8 zilivamiwa.