Na Munir Shemweta, WANMM
Waziri Lukuvi ameagiza kuchukuliwa hatua na kuchunguzwa watendaji wote wa chuo cha ardhi Morogoro (ARIMO) waliohusika kuchelewesha urasimishaji makazi katika kata ya Kivule Dar Es Salaam.

Aidha, Waziri Lukuvi aligiaza pia Makamishna wote wa ardhi katika ofisi za ardhi za mikoa kumpatia majina na kampuni zilizoshindwa kutekeleza kazi za urasimishaji huku zikiwa zimechukua fedha za wananchi.

Lukuvi alitoa maagizo hayo tarehe 8 Machi 2021 alipozungumza na wananchi wa Kata ya Kivule Dar es Salaam alipokwenda kushughulikia kero ya urasimishaji kwenye eneo hilo.

"Watumishi wote waliosababisha kuchelewesha zoezi la urasimishaji hapa Kivule wachukuliwe hatua kali na uchunguzi ufanyike dhidi yao why mwanatutukanisha katika jambo hili" alisema Lukuvi.

Waziri Lukuvi alisema, kilichofanywa katika zoezi hilo hakikufanywa na serikali bali ni majambazi wawili watatu, na wizara yake haiko tayari kuvumilia uhuni uliofanywa. Alizitaka kamati zote za urasimishaji kusimamia vizuri zaezi hilo huku akisisitiza kuwa kazi wanayofanya ni ya kujotolea na siyo ya kujilipa fedha.

Kwa mujibu wa Lukuvi, Wizara yake haiwezi  kuacha zoezi lililopata baraka na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe John Pombe Magufuli halafu iache hivi hivi bila kuchukua hatua dhidi ya watu wachache wanaohujumu.

Alimuagiza katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo kuchukua hatua dhidi ya watumishi wa chuo cha Ardhi Morogoro ambacho kiko chini ya wizara hiyo na kuanza uchunguzi kujua fedha zilizotolewa kwa kazi hiyo zimeenda wapi.

Aidha, Waziri Lukuvi alikiagiza chuo cha ardhi Morogoro kuanza kazi  ya urasimishaji makazi kwa wakazi wote 20,000 wa kata ya Kivule na zoezi hilo likamilike kufikia juni 30 sambamba na kuwataka wananchi waliowekewa alama (Vigingi) kukamilisha malipo ili waweze kupatiwa hati.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Urasimishaji katika kata ya kivule, jumla ya wananchi 3,446 wa kata hiyo wamechangia zaidi ya milioni 534 kwa ajili ya kufanyiwa urasimishaji lakini kazi hiyo imeshindwa kufanyika tangu mwaka 2017 na kati ya hao waliopatiwa hati ni 22 pekee.

"Zoezi limechelewa na waliopewa kazi hiyo wamefanya vibaya sana na kuhoji chuo kinachofundisha wataalam wa ardhi, inakuaje kinaonesha mfano mbaya?" Alisema Waziri Lukuvi.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) Charles Saguda alimuahidi Waziri Lukuvi kukamilisha zoezi la urasimishaji katika kata hiyo inayohusisha mitaa ya Kerezande, Kivule, Magole na Bombambili kufikia juni 30 kama alivyoagiza na tayari wataalamu wapo eneo la tukio na kuanza l kazi.