Na Assenga Oscar

Waziri wa maji Jumaa Aweso amezitaja sababu zilizokuwa zikikwamisha miradi ya maji kuwa ni kutokana na kuwatumia wakandarasi wababaishaji na wasiokuwa na uwezo.

Waziri Aweso ametoa, sababu hiyo wakati akifungua kikao kazi cha wadau wa maji Mkoa wa Tanga kilichofanyika wilayani Lushoto.

Waziri Aweso alisema wakandarasi wasiokuwa na uwezo walikuwa wakipewa zabuni kwa kujuana na hivyo kusababisha kusababisha miradi ya maji kutokamilika na hatua hazichukuliwi.

Alisema wizara hiyo hivi sasa imeondokana na changamoto  hiyo baada ya kuweka mikakati ya kuhakikisha wakandarasi wa namna hiyo hawapati nafasi.

"Wataalamu walikuwa wakijua wazi kuwa baadhi ya wakandarasi walikuwa hawana uwezo lakini bado walikuwa wakiwatumia na kuwaacha wale wenye uwezo,"alibainisha waziri Aweso.

Sababu nyingine iliyokuwa ikikwamisha miradi hiyo ya maji ni michakato isiyokuwa na ulazima ambayo ilikuwa ni kikwazo kikubwa cha ukamilishaji wa miradi mbalimbali nchini.

Aliwaagiza, watendaji kayika, wizara hiyo kuacha visingizio badala yake watekeleze wajibu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigela ameipongeza wizara hiyo ya maji kwa kujitahidi kufikisha maji katika maeneo yaliyokuwa na changamoto kubwa ya maji katika Mkoa Tanga.

Naye Meneja wa Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (Ruwasa)  Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo katika kutekeleza, bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22 Ruwasa Mkoa Tanga inategemea kutumia jumla ya shilingi 38,437,802,839.39 ingawa mahitaji halisi ni shilingi 41,872,700,424.04 ili kukamilisha ujenzi wa miradi inayoendelea.

Alisema miradi hiyo ni pamoja na ukarabati wa miradi chakavu,  usanifu na ujenzi wa miradi mipya.

"Ruwasa Tanga inajumuisha wilaya zake 7 na inategemea kutekeleza ujenzi miradi ya mipya ya maji kukarabati ya zamani kupanua miradi inayoendelea na kusanifu miradi mipya kwa kupitia  bajeti ya mwaka wa fedha 2021/12.

Kikao hicho kilikuwa na lengo la kufanya tathimini pamoja na kuangalia hatua za utekelezaji zilizofikiwa kwenye miradi ya maji.