Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linawashikilia watu wawili wakituhumiwa kwa kosa la kusambaza taarifa za uzushi kwenye mitandao ya kijamii kuwa viongozi wakuu wa serikali ni wagonjwa, kinyume na Sheria ya Makosa ya Mitandao.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Ronald Makona  leo  Jumatatu Machi 15,2021,watu hao walikamatwa kwa nyakati tofauti.


Amewataja watu hao kuwa ni Peter Pius Silayo (30) Mkazi wa Tegeta Dar es Salaam, ambaye alikamatiwa eneo la Kibaoni Tarakea Wilaya ya Rombo na Melchiory Prosper Shayo (36) mkazi wa Keni Wilaya ya Rombo.


Kamanda amesema watuhumiwa watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.


Aidha, Jeshi la Polisi mkoani hapa limetoa wito kwa jamii na wananchi kwa ujumla kuacha kusambaza taarifa ambazo hazina ukweli, na kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa wale watakaobainika.