Watu zaidi ya 20 wamefariki katika milipuko mikubwa iliotokea katika kambi ya jeshi katika mji wa Bata, mji mkuu wa uchumi wa Equatorial Guinea.

Zaidi ya watu 600 walijeruhiwa katika mlipuko huo uliotokea katika ghala la silaha, kulingana na ripoti rasmi ya awali.

Milipuko hiyo imesababishwa na "uzembe" uliohusishwa na hifadhi ya baruti kali kambini, rais wa Eguatorial Guinea amesema.

Rais Teodoro Obiang Nguema amesema katika taarifa kwamba athari iliyotokana na mlipuko huo "imesababisha uharibifu mkubwa wa mali na vitu huko Bata", na kutoa wito kwa jamii ya kimataifa kusaidia.

Waziri wa afya wa Equatorial Guinea ameomba wahudumu wa afya kujitolea na kwenda katika hospitali ya eneo la Bata. Pia imetoa wito watu kujitolea kutoa damu kwasababu ya idadi kubwa ya waliojeruhiwa.