Mahakama kuu ya kanda ya Iringa  iliyofanya kikao chake mkoani Njombe imewahukumu adhabu ya   kunyongwa hadi kufa Watu  5  wa kijiji cha Usalule kilichopo wilayani Wanging’ombe mkoani  humo kwa kosa la kula njama na  kushirikiana kutekeleza mauaji ya  Alice Mtokoma( 56 ) mkazi wa kijiji cha Usalule  huku sababu kubwa ikiwa ni kulipiza kisasi  .

Washtakiwa James Msumule almaarufu Jembe, Emmanuel Ngailo,Izack Ngailo,Anitha Mbwilo na Upendo mligo ambao ni wakazi wa kijiji cha Usalule  wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa  kwa kosa la kuuua kwa kukusudia  chini ya kifungu namba  196 na 197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya 2019 .

Wakisoma shauri la namba 84 ya mwaka 2014  mbele ya jaji wa mahakama kuu , jaji  Firmin Matogolo  mawakili wa serikali  Matiko Nyengelo pamoja  na Andrew  Mandwa wamesema  mnamo tarehe 13 mwezi wa tano  mwaka 2012 katika kijiji cha usalule  washtakiwa walimuua Alice Mtokoma kwa madai ya kulipiza kisasi baada ya kumtuhumu marehemu  Alice kuwa alihusika na kifo cha mume wa mshatakiwa Upendo Mligo.

 Mahakama imeelezwa   kwamba mara baada ya Mume wa Upendo kufariki  dunia ,Upendo kwa kushirikiana na mama mkwe wake  anaejulikana kwa jina la Anita Mbwilo walikwenda kwa mganga ili kujua aliyemuua ndugu yao ,kwa madai kwamba hakufa kifo cha kawaida na kisha kuelezwa kwamba aliyehusika na kifo ni Alice Mtokoma ambaye ni mke mwenza na Anita Mbwilo.

Baada ya mganga kuwatajia mhusika ndipo  Upendo Mligo na Anita Mbwilo wakala njama na kuwatafuta James Msumule almarufu Jembe , Emmanuel Ngailo  Na Izack Ngailo na kisha kuwapa fedha kiasi cha sh. laki tatu ili kutekeleza mauaji ya Alice Mtokoma .

Akisoma adhabu jaji Firmin  Matogolo  amebainisha kuwa washtakiwa wamekutwa na kosa la mauaji ya kukusudia na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa adhabu iliyotolewa chini ya kifungu namba 197 cha kanuni ya adhabu sura namba 16 marejeo ya 2019 ikisomwa pamoja na kifungu namba 322 kifungu kidogo cha kwanza na cha pili cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 marejeo ya mwaka 2019.

 Upande   wa utetezi  wa kesi hii umeongozwa na mawakili Frank Ngafunika, Musa Mhagama ,Tunsume Angumbwike,Innocent Kibadu pamoja naye Octavian Mbungani.