Wataalamu wa usalama wa afya kutoka shirika la Afya Duniani WHO, wanajiandaa kukutana leo kuhusu chanjo ya COVID-19 ya AstraZeneca ambayo imesitishwa katika nchi kadhaa kutokana na hofu ya kusababisha damu kuganda, wasiwasi unaokwamisha vita dhidi ya janga la virusi vya corona mnamo wakati maambukizi ya virusi hivyo yakiongezeka.

Mataifa matatu makubwa ya Umoja wa Ulaya, Ujerumani, Italia na Ufaransa, jana Jumatatu yalisitisha utoaji wa chanjo hiyo, hivyo kuungana na mataifa mengine ambayo pia yamesitisha utoaji wa chanjo hiyo.

Hatua hiyo ni pigo dhidi ya kampeni ya utoaji chanjo ulimwenguni kote dhidi ya ugonjwa huo ambao tayari umewaua zaidi ya watu milioni 2.6. Akizungumzia suala hilo, mkuu wa shirika la Afya Duniani Dr. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema: "Ni suala la kawaida kuchunguza hilo na inaonyesha kwamba mifumo ya ufuatiliaji inafanya kazi na kuna udhibiti imara. 

Kamati ya WHO kuhusu usalama wa chanjo imekuwa ikitathmini data zilizopo na inashirikiana kwa karibu na mamlaka inayosimamia dawa Ulaya na itafanya mkutano nao leo.

"Hata hivyo shirika la Afya Duniani, kampuni ya AstraZeneca pamoja na mamlaka inayosimamia dawa barani Ulaya, zimeshikilia kwamba chanjo hiyo ni salama na kwamba hakuna uhusiano wowote kati ya chanjo hiyo na ripoti hizo za kuganda kwa damu.