Shirika la usimamizi na udhibiti wa dawa barani Ulaya EMA, limesema leo kwamba bado linaamini, manufaa ya chanjo ya virusi vya corona ya AstraZeneca ni mengi kuliko athari zake, licha ya nchi kadhaa kusitisha utoaji wa chanjo hiyo kufuatia hofu kwamba inasababisha damu kuganda. 

Hayo yamesemwa na mkuu wa shirika hilo Emer Cooke alipozungumza na waandishi wa habari kwa njia ya video mchana wa leo, baada ya wataalamu wa shirika hilo kukutana mjini Amsterdam mapema leo kutathmini data za chanjo hiyo.Ameongeza kusema, hakuna ishara kwamba kuganda kwa damu kulisababishwa na chanjo hiyo. 

Dalili hizo hazikujitokeza kwenye majaribio yao wala hazikuorodheshwa kama miongoni mwa athari za kutarajiwa kutokana na chanjo hiyo.Wakati huo huo, wataalamu wa afya wa shirika la afya duniani WHO pia wanatarajiwa kutoa tamko kuhusu chanjo hiyo baadaye leo.

Nchi kadhaa ikiwa ni pamoja na Ujerumani, Ufaransa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, zimesitisha utoaji wa chanjo hiyo kufuatia hofu kwamba inasababisha damu kuganda.