Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wananchi kuacha kutoa lawama kwa serikali kila uharibifu wa miundombuinu unapotokea na kudai kurekebishiwa na badala yake kuwataka kuwa walinzi kwa wale wanaoharibu miundombinu hiyo ili kuisadia serikali kuokoa fedha nyingi katika kurekebisha miundombinu hiyo na hatimae kuzielekeza fedha hizo katika maeneo mengine muhimu.

Mh. Wangabo amesema kuwa kila kukicha shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji Pamoja na kuharibu miundombinu zimekuwa zikipigiwa kelele lakini wananchi wamekuwa wakiziba masikio na kuwafumbia macho wale wanaoihujumu miundombinu hiyo na kuwa mstari wa mbele kuinyooshea kidole serikali kanakwamba wao sio sehemu ya serikali hiyo.

Mh. Wangabo ameyasema hayo katika mkutano na wananchi wa Kijiji cha Kaoze, kata ya Kaoze, Bonde la Ziwa Rukwa, Wilauyani Sumbawanga baada ya wananchi hao kulalamikia ubovu wa barabara hali inayowafanya wananchi hao kushindwa kutoka wala kuingia ndani ya vijiji vyao pale mvua zinapozidi na hatimae mito kujaa na madaraja kusombwa.

“Pamoja na umuhimu wa barabara hiyo nataka mnipe ufumbuzi wa pale (Kijiji cha) Chombe ambapo huwezi kupita pale, tunafanya nini, ukitaka kuwahamisha wale watasema nilipe, nani anawalipa, mtawalipa ninyi wananchi mnaotaka hiyo barabara, tukitaka kupaunganisha pale mchange fedha zenu muwalipe wale halafu muwatoe, halafu hawa TANROAD na TARURA ‘wa-survey’ tuone tunapitisha wapi hiyo barabara,”

“Kwasababu kuna korongo kubwa kwelikweli pale, yaani huwezi kupita pale, tulipita kwabahati bahati pembeni karibu na shamba, halafu tukakutana na ng’ombe na hatukwenda tena mbele, haya ndio yanayotokea huku kwetu, sasa nataka wananchi mnaponipa mimi ombi kama hilo na ninyi mniambie tunafanye pale chombe, mtakaa kwenye WardDC yenu, Diwani we ni Mwenyekiti wa kAmati ya Maendeleo ya Kata, mzungumzie suala hili la uharibifu wa barabara hasa, kulima kwenye vyanzo vya maji lakini pili mifugo, ng’ombe wanatembezwa barabarani wanaharibu barabara,” Alisisitiza.

Aidha, Amesema kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote wanaokiuka sheria na kuwa ipo mbioni kuikabidhi safu ya milima ya Lyamba Lyamfipa Kwa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) baada ya watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kuonekana kushindwa kudhibiti wananchi wanaoharibu mazingira ya safu hizo na hivyo kuendelea kuwaasa wananchi kuacha kuharibu maizingira na vyanzo vya maji kutoka katika milima hiyo.