Wanajeshi wa Nigeria wamepata ruhusa ya kuwapiga risasi bila kuhitaji kibali, watu wote watakaoonekana wakiwa na bunduki aina ya AK-47, kufuatia agizo la rais Muhammadu Buhari. 

Amri hii imetolewa kufuatia kuzorota kwa hali ya usalama, baada ya visa vitatu vya utekaji nyara kati ya Desemba na Februari, ambapo magenge ya wahalifu yaliwachukua mateka mamia ya wanafunzi.

Desemba iliyopita, wavulana zaidi ya 300 walitekwa kutoka shule yao ya bweni katika mji wa Kankara, na mwezi uliopita, idadi kama hiyo ya wasichana walichukuliwa mateka kutoka shule ya Jangebe. 

Wengi wa wasichana hao tayari wamekwishapatikana, lakini wavulana wote hawajulikani walipo. 

Aghalabu, watekaji nyara katika visa kama hivyo huja wakijihami kwa bunduki chapa AK-47, ambazo, kulingana na msemaji wa rais, Femi Adesina, zinaruhusiwa tu kumilikiwa na maafisa wa usalama. Mbali na wanafunzi, wahalifu wenye silaha huwateka pia wasafiri kwenye barabara.