Maroketi saba yamevurumishwa katika kambi ya jeshi la Iraq ya Al-Balad inayotumiwa na wanajeshi wa Marekani kaskazini mwa mji mkuu Baghdad. 

Duru ya usalama imesema shambulizi hilo lililofanywa jana jioni halikusababisha maafa wala uharibifu baada ya maroketi mawili kuilenga kambi hiyo. 

Afisa mmoja wa usalama amesema maroketi mengine matano yalianguka katika kijiji kilicho karibu baada ya yote saba kufyatuliwa kutoka kijiji jirani katika mkoa wa Diyala, mashariki mwa kambi hiyo. 

Hakuna kundi lolote lililodai kuhusika . Mashambulizi kama hayo yamefanywa katika wiki za hivi karibuni yakiyalenga maeneo ambako wanajeshi wa Marekani wanaendesha shughuli zao.