Na: Mwandishi Wetu – Dodoma
Vyama vya wafanyakazi ni kiungo mathubuti kati ya wafanyakazi na Waajiri mahala pa kazi na hivyo vimetakiwa kutekeleza majukumu kwa weledi kadri miongozi iliyo kwenye Katiba na kanuni za kuendesha vyama.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipokuwa akifungua kikao cha viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri na Wadau wa Sekta ya Usafirishaji kilichofanyika  Machi 10, 2021 katika ukumbi wa mikutano uliopo ghorofa ya PSSSF, Jijini Dodoma.

Waziri Mhagama alieleza kuwa, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini imeainisha majukumu ya Vyama  vya wafanyakazi na wajibu wa  mwakilishi wa vyama kwa wanachama ikiwemo suala la kutoa huduma bora kwa wanachama, namna ya kuwapata wanachama, kuhakikisha mwajiri anatekeleza Sheria na kushauri kuhusu mahusiano mema mahala pa kazi.

“Katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kumekuwa na utulivu wa kutosha ambao umepelekea vyama vya wafanyakazi chini ya uongozi wa shirikisho na uongozi wa vyama vyenyewe kujipanga vizuri na kutumika kama daraja kati ya waajiri na wafanyakazi,” alieleza Mhagama

“Suala hili litawezesha vyama kuwa na tija na kushiriki kikamilifu katika kukuza ustawi na usalama wa wafanyakazi na waajiri mahala pa kazi,” alisema

Alieleza kuwa Sekta ya Usafirishaji ni muhimu katika ujenzi wa uchumi wa taifa, hivyo Serikali itaendelea kuthamini mchango wa sekta ya usafirishaji nchini na kufanya kila linalowezekana kwa wafanyakazi katika sekta hii kufurahia mchango wao na waajiri kushiriki kikamilifu katika kukuza sekta hii muhimu.

Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikishughulikia malalamiko na migogoro mingi inayoigusa sekta hiyo lengo ikiwa ni kuhakikisha sekta hiyo panakuwa eneo bora linaloleta tija.

“Tunatambua kuwa Sheria zatu za kazi zinazotukutanisha katika dhana ya utatu yaani Serikali, Mwajiri na Mfanyakazi ili kuwa na majadiliano na mashauriano ya pamoja katika kutafuta shuluhisho la changamoto zilizopo, hivyo nimeona ni vema leo tukutane na tuzungumze kwa kina ili kutafuta suluhu na kuondoa migogoro katika sekta hii,” alieleza Mhagama

Aliongeza kuwa ofisi yake imekuwa ikifanya vikao mbalimbali na viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri na Wadau wa Sekta ya Usafirishaji na kwa pamoja waliandaa Mpango kazi wa kushughulikia kero zinazoikabili sekta hiyo.

Aidha Waziri Mhagama aliwataka viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri na Wadau wa Sekta ya Usafirishaji kuendelea kushirikiana na Ofisi yake na kushauri namna mbalimbali za kuboresha sekta hiyo kwa kwa wao ndio watekelezaji wa majukumu ya kila siku katika sekta ya usafirishaji nchini.

Waziri Mhagama alitoa wito kwa Vyama vya Wafanyakazi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Katiba na Kanuni pamoja na kuzingatia madhumuni ya kusajiliwa kwako.

“Ninaamini kuwa iwapo vyama vya wafanyakazi vitatekeleza majukumu yao kwa weledi, vitakuwa imara kushauri na kuwawakilisha wafanyakazi na kusogeza maoni yao kwenye vyombo mbalimbali vya maamuzi nchini,” alisema

Kwa Upande Wake, Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri Bi. Pendo Berege alisema kuwa majadiliano yatakayofanyika kwenye kikao hicho itakuwa njia nzuri ya migogoro kupungua na wadau wote wataweza kushirikina vizuri ili kuwa na mahala pa kazi kunakozingatia viwango vya kazi na kuleta tija.