Na Stella Kalinga, Simiyu RS.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka ametoa rai kwa Viongozi wa Serikali mkoani hapa kutumia busara na akili badala ya kutumia nguvu katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi katika maeneo waliyopo na kuhakikisha ufumbuzi unaotolewa unaleta tija kwa wananchi.

Mtaka ametoa rai hiyo wakati akifungua  kikao maalum cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) , kilichofanyika Machi 13, 2021 Mjini Bariadi kwa lengo la kupitia Rasimu ya Mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Mkoa wa Simiyu ya mwaka 2021/2022.

“Wito wangu kwa viongozi wenzangu tupunguze kutumia nguvu, tuongeze matumizi ya akili tuone matokeo kwa wananchi wetu, leo tunapitisha mapendekezo ya bajeti ya mkoa mwaka 2021/2022 lakini ningetamani kuona miradi mipya ya Halmashauri inayogusa watu, halmashauri zetu zijielekeze kwenye kuanzisha miradi ambayo itakuwa vyanzo vipya vya mapato,” alisema.

Aidha, Mtaka ametoa rai kwa Viongozi wa Mkoa na Halmashauri kupima tija ya vikao vyao na kuhakikisha vikao wanavyokaa vinaleta tija ikiwa ni pamoja na namna vikao hivyo vinavyosaidia kubuni na kuongeza vyanzo vya mapato.

Akiwasilisha mapendekezo ya rasimu ya mpango na bajeti ya Mkoa wa Simiyu, Katibu Tawala Msaidizi-Sehemu ya Mipango na Uratibu, Bw. Donatus Weginah amesema katika mwaka wa fedha 2021/2022 Simiyu inatarajiwa kutengewa shilingi bilioni 200.5 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, mishahara na matumizi mengineyo.

Akizungumza kwa niaba ya wabunge  Mwenyekiti wa Wabunge wa mkoa wa Simiyu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kisesa ameunga mkono mapendekezo ya mpango na bajeti ya mkoa na kuahidi ushirikiaono wa wabunge hao katika kupitisha bajeti hiyo bungeni.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga ametoa wito kwa kwa viongozi wote mkoani Simiyu kushirikiana na vyombo vinavyohusika na usimamizi wa fedha kudhibiti na kusimamia matumizi ya fedha zote za Serikali ili ziweze kuleta tija.

Akitoa salamu kwa naiba ya Chama cha Mapinduzi, Katibu wa CCM mkoa wa Simiyu, Bi. Haula Kachwamba amewashauri wataalam kila mmoja kutimiza wajibu wake katika kubuni vyanzo na mbinu za kuongeza mapato kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa mkoa wa Simiyu .