Viongozi mbalimbali wa kisiasa wametoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Rais John Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ametangaza kifo cha Rais Magufuli saa tano usiku wa kuamkia leo  akisema kimetokana na tatizo la moyo la mfumo wa umeme ambalo alikuwa nalo kwa zaidi ya miaka 10.

Katika ukurasa wake wa Twitter, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameandika, “kwa masikitiko makubwa Machi 17, 2021 saa 12 jioni tumempoteza Rais John Magufuli ambaye amefariki kwa maradhi ya moyo katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu. Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.”

Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe naye ametoa salamu zake za rambirambi akieleza kupokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Rais Magufuli huku akitoa pole kwa mama Janeth Magufuli pamoja na familia yake.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa naye ameandika katika ukurasa wake wa Twitter: “Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe. Amina.”
 
Wengine waliotoa salamu za Pole ni Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson,Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi,Rais wa Somalia Mohamed Farmaajo,Rais wa Venezuela Nicolás Maduro 

Mbali na salamu hizo za watu mbalimbali, vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi vimeripoti taarifa ya kifo

Rais Magufuli amefariki akiwa na umri wa miaka 61 akiwa ametawala kwa miaka karibu sita tangu alipochaguliwa katika uchaguzi wa Oktoba 2015. Pia, alishinda uchaguzi wa Oktoba 28 mwaka jana kwa muhula wake wa pili ambao hajaumaliza.

Mama Samia ametangaza siku 14 za maombolezo ya kifo chake ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti wakati taratibu za mazishi zikiandaliwa.