Samirah Yusuph.

Itilima. Wananchi wa Wilaya ya itilima mkoani Simiyu wanatarajia kunufaika na Mradi wa kutoa ajira za muda kwa walengwa wa TASAF chini ya mpango wa kunusuru kaya masikini katika awamu ya tatu kipindi cha pili.

Mradi umelenga kuvifikia vijiji 55 kati ya vijiji 102 vya wilaya hiyo, ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miezi sita katika kila kijiji hali itakayo sababisha walengwa wa eneo husika kupata ajira za muda kwa kipindi chote cha mradi.

Hayo yameelezwa na afisa ufuatiliaji TASAF Wilaya ya Itilima Paulo Tibabihilila wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa timu ya wawezeshaji ngazi ya mamlaka ya eneo la utekelezaji kuhusu maandalizi, utekelezaji na usimamizi wa mradi.

Amesema kuwa zoezi la kuibua miradi katika vijiji limeanza katika hatua ya awali ya mafunzo kwa wawezeshaji ili waweze kwenda kubaini miradi itakayokuwa na tija  katika jamii na kuwa utekelezaji wake utatumia teknolojia rahisi pamoja na nguvu kazi ya wananchi.

"Miradi itaibuliwa na wananchi wenyewe, wataitekeleza katika hatua zote za utekelezaji na baada ya kukamilika wataisimamia...

Lengo likiwa ni kutengeneza miundo mbinu mizuri katika jamii pamoja na kuwapa wananchi ujuzi katika kuendesha miradi ili waondokane na umasikini".

Akielezea miradi ambayo itakwenda kutekelezwa katika vijiji mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo Skay Thomas amesema kuwa miradi itakayokwenda kutekelezwa ni pamoja na miradi ya upandaji miti, miradi ya maji, barabara, umwagiliaji pamoja na kuongeza rutuba ya udongo.

Huku baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo Maiko Mhoja na Mary Boniphace wakieleza kuwa mradi huu umekuwa na mapokeo chanya kwa sababu umelenga kuinufaisha jamii.

"Muhimu ni kupeleka elimu katika jamii ili waweze kuwa tayari kuipokea na kuiendele za miradi kwa manufaa yao".  

Aidha mkurugenzi mtendaji wa halshauri ya wilaya ya Itilima Elizabeth Gumbo Amewataka wawezeshaji kwenda kuibua miradi endelevu katika vijiji ili hata baada ya mradi kuisha wananchi waendelee kuwa na uwezo wa kuiendeleza miradi hiyo.

Halmashauri ya wilaya ya Itilima ni miongoni mwa halmashauri 51 nchini ambazo zinanufaika na mradi wa ajira kwa muda, mlengwa atapata nafasi ya kuajiriwa kwa kipindi cha miezi sita, katika siku 30 za mwezi atafanya kazi siku 10 kwa masaa manne kwa siku.


Mwisho.