Idadi ya vifo kutokana na COVID-19 barani Ulaya imepindukia watu 900,000. Hayo ni kulingana na takwimu za mamlaka za afya zilizojumuishwa na shirika la habari la AFP.

Idadi hiyo inalifanya bara la Ulaya kuwa lililoathirika zaidi baada ya kusini mwa Amerika na nchi za Karibea ambazo zimesajili jumla ya vifo 721,581 na pia mbele ya Marekani na Canada ambazo zimerekodi vifo 558,110 kutokana na virusi vya corona tangu janga hilo lianze Disemba 2019 nchini China.

Hapo jana idadi ya maambukizi ya virusi hivyo barani Ulaya pia ilipindukia watu milioni 40.Uingereza ndilo taifa lililoathiriwa zaidi Ulaya likiwa limerekodi jumla ya vifo vya watu 125, 580, miongoni mwa jumla ya watu 4, 263, 527 walioambukizwa.

Ulimwenguni kote, zaidi ya watu milioni 120 wameambukizwa virusi vya corona na takriban watu mioni 2.66 wameshaaga dunia kufuatia janga hilo.