Ikulu ya Kremlin imekanusha kuwa Urusi na China zinatumia chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 kama njia za kupanua ushawishi wao kijiografia, baada ya shutma kuwa nchi hizo zinatumia chanjo kuimarisha ushawishi wao katika sehemu nyengine duniani. 

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amewaambia waandishi wa habari kuwa hakubaliani na madai kuwa Urusi na China zinaanzisha vita vya aina fulani duniani, na kwamba nchi hizo mbili hazitumii suala la chanjo kama njia ya kupanua ushawishi wao.

Mapema Ijumaa, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alidai kuwa nchi yake inakabiliwa na "aina mpya ya vita vya ulimwengu" na kunyoosha kidole cha lawama kwa Urusi na China kwa kutumia suala la chanjo kuimarisha ushawishi wao duniani.

Hata hivyo, Urusi na China zimeshtumu nchi za Magharibi kwa kujilimbikizia akiba nyingi za chanjo badala ya kuzisambaza kwa mataifa maskini.