Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binaadamu Michelle Bachelet amesema kiasi ya watu 54 wameuawa na zaidi ya 1,700 kukamatwa tangu mapinduzi ya kijeshi ya Februari mosi nchini Myanmar. 

Matamashi yake yamekuja baada ya siku mbaya kabisa ya umwagaji damu katika maandamano ya Myanmar, ambapo karibu watu 38 waliuawa jana katika maandamano ambayo vikosi vya usalama vilionekana vikiwafyatulia risasi waandamanaji. 

Bachellet amelitaka jeshi kuwacha kusitisha ukandamizaji wake dhidi ya waandamanaji wenye amani. Karibu watu 700 walikamatwa jana pekee huku wengi wao wakichukuliwa katika kamatakamata ya jeshi na polisi. 

Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya umesitisha miradi yote ya maendeleo nchini Myanmar ili kuepusha msaada wa kifedha kwa jeshi baada ya kukamata madaraka mwezi uliopita. 

Halmashauri Kuu ya Ulaya imethibitisha kuwa imesitisha msaada wa kifedha, ambao katika miaka iliyopita ulihusisha zaidi ya euro milioni 200 katika mipango tofauti inayotekelezwa aghalabu kwa miaka minne.