Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel amesema leo kuwa vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi kutokana na jinsi inavyomtendea kiongozi wa upinzani Alexei Navalny vinaonesha kuwa umoja huo umeungana katika kutetea maslahi yake.
Awali ikulu ya Urusi, Kremlin ilikuwa imepuuza athari za vikwazo vilivyowekwa na Marekani na umoja huo lakini ikasema italipiza na hatua kama hizo. Michel ameongeza kuwa waliamua kuweka vikwazo kwa sababu ya kesi dhidi ya Navalny.
Michel alikuwa akizungumza mjini Kyiv akiwa pamoja na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy aliyetoa wito kwa Umoja wa Ulaya kuweka vikwazo zaidi vinavyohusiana na ukiukaji wa haki za binadamu katika eneo la Crimea lililotwaliwa kwa nguvu na Urusi mnamo mwaka 2014.
Zelensky amesema kuwa haamini kurudiwa kwa mahusiano ya kawaida kati ya Umoja wa Ulaya na serikali ya shirikisho ya Urusi bila ya kudumisha uadilifu wa kimipaka na taifa lao.