Mkuu wa taasisi ya Robert Koch inayoshughulikia magonjwa ya kuambukiza nchini Ujerumani ameonya kuwa huenda wimbi la tatu la virusi vya Corona likawa baya zaidi kwa nchi hiyo.

Lothar Wieler amesema pia sio ajabu kwa nchi hiyo kurekodi maambukizi mapya 100,000 kwa siku na kuwahimiza watu kusalia majumbani wakati wa sikukuu ya Pasaka.

Idadi ya maambukizo mapya nchini Ujerumani imeongezeka katika wiki za hivi karibuni, maambukizo hayo mapya yakisababishwa na aina mpya ya kirusi cha Corona kinachosambaa kwa kasi pamoja na kulegezwa kwa baadhi ya vizuizi.

Waziri wa afya Jens Spahn ameonya kuwa mfumo wa afya wa Ujerumani huenda ukalemewa kufikia mwezi Aprili.Idadi ya maambukizo mapya ya ugonjwa wa Covid-19 imeongezeka kwa visa 21, 573 kufikia leo Ijumaa huku idadi ya watu waliokufa kwa ugonjwa huo ikiongezeka kwa 183.