Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amebadilisha uamuzi wake wa kuzuia shughuli za kiuchumi katika kipindi cha msimu wa sikukuu ya Pasaka, uliokuwa umelenga kudhibiti kuenea maambukizo ya virusi vya Corona. 

Duru zimeliambia shirika la habari la kijerumani dpa kwamba hatua ya kubadili uamuzi huo,imechukuliwa baada ya kauli za kuukosoa kuongezeka.

Kansela Merkel ameuleza mkutano leo kwamba uamuzi wa mwanzo uliofikiwa mwanzoni mwa wiki hii wa kufunga maduka mengi zaidi nchini Ujerumani na kupigwa marufuku mikusanyiko kuanzia tarehe 1 hadi 5 Aprili hautatekelezwa. 

Kiongozi huyo wa Ujerumani amekiri kufanya kosa na kuomba radhi.Tangazo hili jipya limesababisha mkanganyiko kuhusu mkakati wa serikali wa kupambana na janga la virusi hivyo.