Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amezindua mipango ya kulegeza taratibu vizuizi vya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona katika taifa hilo kubwa kiuchumi barani Ulaya. 

Merkel na mawaziri wakuu wa majimbo 16 ya shirikisho la Ujerumani wametangaza mpango wa hatua kwa hatua wa kulegeza vizuizi, ikiwa ni pamoja na kufungua biashara licha ya wasiwasi kuhusiana na kusambaa kwa aina mpya ya virusi vinavyosambaa kwa kasi, baada ya Kansela huyo kuzidiwa na shinikizo la kisiasa na kutoridhika kwa umma kuhusu janga hilo. 

Mpango huo utatekelezwa hatua kwa hatua na vizuizi vingi vilivyopo kwa sasa vitaendelea kutekelezwa hadi Machi 28, lakini kuanzia Jumatatu ijayo, Wajerumani wataruhusiwa kukutana zaidi, huku watu watano kutoka kaya mbili wakiruhusiwa kukutana.