Na Mwandishi wetu,
Serikali ya Ufaransa imeahidi kutoa Euro milioni 150 sawa na shilingi za kitanzania kwa ajili ya kuendeleza mradi wa awamu ya tano wa ujenzi wa mradi wa mabasi ya mwendokasi jijini Dar es Salaam.

Ahadi hiyo imetolewa na Balozi wa Ufaransa hapa nchini, Mhe. Frederic Clavier wakati alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi, (Mb) katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Prof. Kabudi amesema kuwa mazungumzo yake na Mhe. Clavie yalijikita katika utekelezaji wa mambo waliyokubaliana wakati alipofanya ziara ya kikazi mwezi Februari nchini Ufaransa.

“Leo katika mazungumzo yangu mimi na Mhe. Balozi tumejadili mambo mbalimbali likiwemo suala la Shirika la Maendeleo la Ufaransa kutoa fedha kwa ajali ya kuendeleza mradi wa awamu ya tano wa ujenzi wa mradi wa mabasi ya mwendokasi jijini Dar es Salaam,” Amesema Prof. Kabudi

Pamoja na mambo mengine, Prof. Kabudi amesema kuwa wamejadili kuhusu miradi ya maendeleo katika sekta ya nishati, maji, afya na kilimo.

“Pia tumejadili kuhusu ushiriki wa Ufaransa katika kuisaidia Tanzania katika uchumi wa buluu, ambapo Shirika la Maendeleo la Ufaransa limeahidi kusaidia Tanzania bara na Zanzibar katika kuendeleza uchumi wa buluu na hasa kuongeza uwezo wa Tanzania kuvua na kuchakata samaki,” Ameongeza Prof. Kabudi.

Kwa upande wake Balozi wa Ufaransa Nchini, Mhe. Frederic Clavier amesema kuwa kikao chake na Mhe. Waziri ni mwanzo wa hatua mpya ya ushirikiano kati ya Tanzania na Ufaransa.

“Nchi ya Tanzania ni nchi ya demokrasia na amani,ambapo inatoa fursa ya kuwekeza katika miradi ya maendeleo, Ufaransa itaendelea kuwa pamoja na Tanzania katika kuhakikisha kuwa inasonga mbele kimaendeleo,” Amesema Balozi Clavie

Katika tukio jingine Prof. Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya hapa nchini, Mhe. Manfredo Fanti na kujadili mambo mbalimbali ya kuboresha ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Tanzania hasa kufuatia utiaji saini wa miradi sita itakayopata uhisani wa fedha kutoka Umoja wa Ulaya.

“Tumekubaliana kuimarisha uhusiano wetu katika maeneo mbalimbali ikiwemo, maeneo ya viwanda, na kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara Tanzania, katika masuala ya mabadiliko ya tabia nchi, kilimo, maji, miundombinu katika kuhakikisha kuwa Tanzania inaongeza uwezo wake wa kuazilisha Nnishati.

Kwa upande wa, Balozi wa Umoja wa Ulaya Mhe. Fanti amesema kuwa pamoja na mambo mengine, wamejadili mambo ya kuboresha uhusiano wa kidiplomasia uliopa baina Umoja wa Ulaya na Tanzania.