Mchakato wa kuwachagua majaji wa kusikiliza kesi ya aliyekuwa afisa wa polisi katika mji wa Minneapolis Derek Chauvin anayeshtakiwa kwa mauaji ya George Floyd ulisimamishwa kabla ya kuanza hapo jana katika juhudi za serikali za kuongeza shtaka la mauaji ya kiwango cha tatu.

Huku mamia ya waandamanaji wakiwa wamekusanyika nje ya mahakama wakitoa wito wa kushtakiwa kwa Chauvin, jaji Peter Cahill alisema kuwa hana uwezo wa kuamua iwapo shtaka hilo la mauaji ya kiwango cha tatu linapaswa kurejeshwa wakati limekatiwa rufaa. 

Awali jaji Cahill alikuwa ameamua kuendelezwa kwa mchakato huo wa kuwachagua majaji kama ilivyopangwa lakini baada ya waendesha mashataka kuiomba mahakama ya rufaa kusimamisha kwa muda kesi hiyo, jaji huyo aliahirisha shughuli hiyo. 

Baadaye jaji Cahill alisema kuwa shughuli hiyo itaendelea Jumanne na kuzuia amri kutoka kwa mahakama ya rufaa.

Hakukuwa na dalili kuhusu wakati mahakama itatoa uamuzi, lakini hatua hiyo huenda ikachelewesha kesi hiyo dhidi ya Chauvin kwa wiki kadhaa.