Aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump ameweka wazi uwezekano wa kuwania tena kwenye kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2024 na kumshambulia mrithi wake Joe Biden, kutoka chama cha Democratic huku akirejelea madai yake yasio kuwa na msingi kwamba aliibiwa uchaguzi wa mwezi Novemba 2020.

Akionekana kwa mara ya kwanza kwa umma tangu aondoke madarakani, karibu wiki sita zilizopita, Donald Trump alionyesha nia yake ya kupeperusha bendera ya Chama cha Republican katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2024;

Akizungumza katika mkutano wa kisiasa wa muungano wa kihafidhina CPAC, Conservative Political Action Conference, uliofanyika mjini Orlando katika jimbo la Florida, Donald Trump alisema huenda akajitosa katika kinyang'anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Trump anadai kuwa uchaguzi wa mwezi Novemba ulikumbwa na udanganyifu mkubwa lakini hajawahi kutoa ushahidi wowote kuunga mkono madai yake.

-RFI