SIKU YA KIMATAIFA YA
WANAWAKE – 2021

 Siku ya Kimataifa ya Wanawake (International Women’s Day) huadhimishwa Machi 8 ya kila mwaka. Siku hii ambayo imekuwa ikiadhimishwa na nchi za Urusi kuanzia mwaka 1917 ilitangazwa na Umoja wa Mataifa kuwa SIKU YA KIMATAIFA YA WANAWAKE kuanzia mwaka 1975.  Siku hii inalenga kutambua mafanikio ya mwanamke bila kuangalia rangi yake, dini, kabila au siasa ikiwa ni pamoja na kutafakari maendeleo ya mwanamke na namna ya kuendelea kujikwamua katika matatizo na changamoto zinazokuwa vikwazo vya yeye kujitegemea kifikra na kiuchumi.

 Kwa kutambua umuhimu wa siku hii pamoja na umuhimu wa mchango wa mwanamke katika mapambano dhidi ya rushwa, Machi 7, 2019, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ilitoa TAMKO kwamba inaunga mkono juhudi zinazoendelea duniani kote za kuhakikisha wanawake wanalindwa na inapinga unyanyasaji na udhalilishaji wa aina yoyote ile unaofanywa dhidi ya wanawake ikiwemo kulazimishwa kutoa RUSHWA YA NGONO. Hii ni hatua muhimu kwa TAKUKURU na JAMII katika harakati za KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA.

 RUSHWA YA NGONO ni kitendo cha mtu kutumia madaraka au dhamana aliyopewa kuomba au kulazimisha tendo au upendeleo wa kingono kutoka kwa mtu anayetaka kumhudumia kikazi. Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007 imetamka kosa hili chini ya kifungu cha 25 ambapo kwa tafsiri isiyo rasmi kifungu hiki kinasema:

 “Mtu yeyote ambaye kwa kutumia nafasi yake au mamlaka yake katika kutekeleza majukumu yake anadai au analazimisha upendeleo wa kingono au upendeleo mwingine wowote kama kigezo cha kutoa ajira, kupandisha cheo, kutoa haki au upendeleo wowote unaotambulika kisheria atakuwa ametenda kosa.”

 Tofauti na aina nyingine za rushwa zinazotumia ubadilishaji wa vitu yakinifu au ridhaa ya mtoa rushwa na mpokea rushwa, hii ni rushwa inayotokana na tabia ya mdai rushwa kutumia mamlaka yake kushawishi au kushinikiza ngono badala ya vitu yakinifu.

 Pamoja na TAMKO tulilolitoa, kwa mujibu wa kifungu cha 7 (a) na (c) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007, TAKUKURU inao wajibu wa kufanya uchambuzi na kupitia taratibu za mamlaka ya umma na binafsi kwa nia ya kuiwezesha kubaini mianya ya vitendo vya rushwa, na kushauri namna bora ya kuziba mianya iliyobainika, na kushirikiana na wadau kupambana na rushwa.

 Hivyo basi, kwa kutambua kuwa Vyuo Vikuu ni viwanda vya kuandaa wataalamu wanaotarajiwa kuingia kwenye fani mbalimbali za utoaji wa huduma, uzalishaji pamoja na kuwa walezi wa familia, TAKUKURU ilifanya utafiti wa kina katika Chuo Kikuu cha Dodoma na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwezi Februari 2020. Lengo kuu la utafiti wetu lilikuwa ni kupata taarifa za kisayansi zitakazosaidia kukabiliana na kero ya rushwa ya ngono katika Taasisi za Elimu ya juu nchini.

MATOKEO YA UTAFITI:

Matokeo ya utafiti yalibainisha mambo yafuatayo:

Mosi, tatizo la rushwa ya ngono kwenye vyuo tafitiwa lipo; wanafunzi asilimia 58 na watumishi asilimia 69 walieleza kuwepo kwa matukio ya vitendo vya rushwa ya ngono;

 Pili, utafiti ulibaini sababu za kuwepo kwa rushwa ya ngono katika taasisi tafitiwa ni kutokana na mifumo dhaifu ya kudhibiti matumizi mabaya ya mamlaka; mifumo dhaifu ya kusimamia uwajibikaji; mfumo dhaifu wa ajira hasa ajira za wahadhiri; kuwa na ufinyu wa huduma muhimu kama hostel na mikopo ya elimu; kuongezeka kwa wanafunzi pamoja na mmomonyoko wa maadili kwa ujumla;

 

Tatu, utafiti ulibaini mbinu zinazotumika kushawishi rushwa ya ngono ambazo ni kutoa alama za chini kwenye mitihani, vitisho vya kutofaulu kwa wanafunzi, kutoa ahadi kama kumpatia ajira, cheo, chumba chuoni, nafasi ya uongozi, kuongezea alama za ufaulu au kusaidia kupata ufadhili wa masomo, kuchelewesha utoaji wa huduma na wahadhiri kuwaita wanafunzi kwenye mazingira yasiyo rasmi kwa ajili ya kukagua kazi zao;

Baada ya kufanya utafiti huu TAKUKURU iliitisha kikao kazi cha wadau cha kujadili matokeo ya utafiti na kuweka mikakati ya kuidhibiti kero hii. Vilevile, tulitoa mapendekezo kwa Serikali pamoja na Taasisi za Elimu ya Juu kuhusu namna ya kudhibiti kero hii katika eneo hili.

Pamoja na utafiti huu, kwa kutambua athari za rushwa ya ngono kwa wahanga, jamii na hata uchumi, TAKUKURU kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Women Fund Tanzania (WFT) Oktoba 2019 tulizindua kampeni iitwayo: VUNJA UKIMYA KATAA RUSHWA YA NGONO. 

Kampeni hii inafanyika katika mikoa yote 28 ya TAKUKURU na inalenga kuelimisha na kuuhamasisha zaidi umma kuwa na ujasiri wa kutoa taarifa na kupinga vitendo vya rushwa ya ngono nchini. Tunashukuru kwamba mwitikio ni mkubwa na imekuwa ni ajenda inayozungumziwa kwa wingi katika jamii.

 WITO WANGU KWA JAMII ni kwamba TAKUKURU tuko imara na tumejipanga vizuri katika kushughulikia kero hii.

·        Tunaendelea kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa baada ya kufanya utafiti katika vyuo vikuu.

 ·        Tunaendelea kutoa elimu dhidi ya rushwa kupitia vipindi vya redio, kufanya semina na pia kupitia vipindi mbalimbali vya televisheni.

 ·        Tumeweka utaratibu maalum wa kushughulikia malalamiko ya kero ya Rushwa ya Ngono katika kila mkoa na kila Wilaya hapa nchini.

 ·        Tumepanua wigo wa mawasiliano yetu na wananchi ambapo sasa TAKUKURU imeanzisha TAKUKURU TV na pia imefungua kurasa za Tweeter: TAKUKURU.TZ; Instagram: takukuru.tz na Facebook: Takukuru Tz.

 Ninawasihi wananchi kutumia fursa hizi kuwafichua wadhalimu wanaodai RUSHWA YA NGONO na rushwa nyingine ili kwa ushirikiano huo tukomeshe vitendo hivyo.

 Kwa maelezo hayo na kwa kuadhimisha SIKU YA KIMATAIFA YA WANAWAKE kwa mwaka 2021, yenye Kauli Mbiu isemayo ‘WANAWAKE KATIKA UONGOZI: CHACHU KUFIKIA DUNIA YENYE USAWA’ Mkurugenzi Mkuu na watumishi wote wa TAKUKURU tunasema: ‘BADILI FIKRA, RUSHWA YA NGONO HAIKUBALIKI - TUWAUMBUE’.


(J.J. Mbungo, ndc)

Brigedia Jenerali

MKURUGENZI MKUU WA TAKUKURU

MACHI 8, 2021