Wanamgambo wa Taliban wametishia kuanzisha tena mashambulizi dhidi ya vikosi vya Marekani ikiwa havitaondoka Afghanistan ifikapo Mei 1. 

Hatua hii inajiri baada ya rais wa Marekani Joe Biden wiki hii kutoa ratiba isiyo wazi juu ya lini wanajeshi wa Marekani wataondolewa Afghanistan. 

Katika taarifa yake Taliban imedokeza kuwa wajibu wote wa kuongezeka kwa vita, vifo na uharibifu utakuwa juu ya wanaokiuka agizo hilo. 

Tarehe ya mwisho ya kuondolewa kwa vikosi vya kijeshi ni sehemu ya makubaliano ya utawala wa Marekani chini ya rais wa zamani Donald Trump aliposaini mkataba na Taliban mwaka jana huko mjini Doha, Qatar. 

Siku ya Alhamisi Biden alisema haoni uwezekano wa Jeshi la Marekani kuendelea kuwepo Afghanistan katika mwaka ujao. Taliban wamesema matamshi ya Biden hayaeleweki na wamesisitiza kwamba makubaliano ya Doha ni chaguo bora la kumaliza vita vya miaka 20, na kuongezea kuwa kundi hilo limejitolea pakubwa kulingana na makubaliano hayo.

DW