Na. Edward Kondela
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema serikali imeweka lengo la kuhakikisha Sekta ya Uvuvi kupitia ufugaji samaki inazalisha idadi kubwa ya samaki sambamba na samaki wapatikanao kwenye maji ya asili.

Akizungumza jana (10.03.2021) alipokuwa akikagua shughuli zinazofanywa na Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji cha Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro, Waziri Ndaki amesema tasnia ya ufugaji samaki imekuwa na mwitikio mkubwa kwa sasa kutokana na mahitaji ya soko la samaki kuongezeka hivyo jitihada nyingi zinafanyika kuongeza uzalishaji wa vifaranga vya samaki.

“Kwa sasa tasnia ya ufugaji samaki imekuwa ikitoa faida kubwa kwa wanaojishulisha na ufugaji hivyo natoa wito kwa watu kujitokeza kwa wingi kufuga samaki  na pia na toa wito kwa vituo vyetu vya ukuzaji viumbe maji vilivyopo nchini kuhakikisha vinaongeza uzalishaji wa samaki kwa kuwa mahitaji ya vifaranga ni mengi.” Amesema Mhe. Ndaki

Aidha, amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi itahakikisha inaendelea kuviboresha vituo hivyo kwa kuboresha miundombinu ya uzalishaji vifaranga na kupanua uwezo wake ili viweze kwenda sambamba na mahitaji ya vifaranga kwa watu wanaofuga samaki.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazael Madalla amesema wizara ipo katika hatua mbalimbali ya kupata programu maalum ya simu ya mkononi itakayoweza kutumiwa na watu wanaotaka kufahamu mambo mbalimbali kuhusu ufugaji samaki na namna ya kupata vifaranga vya samaki kutoka katika vituo ambavyo vipo chini ya wizara.

Pia, Dkt. Madalla amemfahamisha Waziri Ndaki uboreshaji ambao unafanyika katika Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji cha Kingolwira kwa kupanua shughuli za uzalishaji wa vifaranga vya samaki aina ya sato na pia kituo kipo mbioni kuanza uzalishaji wa vifaranga vya samaki aina kambale.

Kuhusu bei ya vifaranga vya samaki amesema kwa sasa vituo vya ukuzaji viumbe maji vilivyo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi vinauza kifaranga kimoja cha samaki aina ya sangara kwa Shilingi 100 na vimekuwa vikiwarahisishia wahitaji wa vifaranga kuwafikishia popote walipo bila ya ulazima wa wao kufika katika vituo hivyo.  

Naye Kaimu Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Ukuzaji Vumbe Maji Kingolwira Bw. Hamady Makorwa amesema mikakati ya kituo katika kuendeleza shughuli za uzalishaji ni kufikia uzalishaji wa vifaranga 600,000 kwa mwezi hivyo kituo kinahitaji mabwawa yasiyopungua 26 na sato wazazi wasiopungua 24,000 ambapo kwa sasa wapo 5,430.

Amefafanua kwa sasa vifaranga vya samaki vilivyopo katika kituo hicho ni 38,000 huku tayari wamepokea maombi ya vifaranga zaidi ya 180,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amefika kwa mara ya kwanza katika Kituo cha Uzalishaji Viumbe Maji cha Kingolwira lengo likiwa ni kuhakikisha tasnia ya ufugaji samaki inakuwa kwa uwepo wa idadi kubwa ya upatikanaji wa vifaranga vya samaki nchini vitakavyouzwa kwa bei nafuu zaidi.