Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema leo kuwa hakuna sababu ya kusitisha matumizi ya chanjo ya virusi vya corona ya AstraZeneca, baada ya mataifa kadhaa ya Ulaya kuzuia utoaji wake kutokana na wasiwasi kuwa inasababisha kuganda kwa damu. 

Msemaji wa WHO, Margaret Harris, amewaambia waandishi habari mjini Geneva kuwa chanjo ya AstraZeneca iliyotengezwa Uingereza ni salama kama zilivyo chanjo nyingine zinazotumika kupambana na janga la Corona. 

Amesema shirika hilo limedurusu data za vifo na hadi leo hakuna kifo hata kimoja kinachohusishwa na chanjo za virusi vya corona wala uhusiano kati ya chanjo ya AstraZeneca na kuganda kwa damu. 

Msimamo wa WHO unafuatia uamuzi wa mataifa kadhaa duniani, yakiwemo ya Ulaya, kusitisha matumizi ya chanjo ya AstraZeneca baada ya ripoti kwamba watu kadhaa waliopatiwa chanjo hiyo walibainika kupata tatizo la kuganda kwa damu.