Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Aboubakar Kunenge amepiga marufuku sherehe zote mkoani humo katika kipindi chote cha siku 21 ambazo Taifa litakuwa likiomboleza kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli.

Kunenge ametoa agizo hilo wakati wa mkutano.wake na Waandishi wa habari mkoani Dar es salaam.

Amesema Watanzania kwa sasa wapo katika majonzi makubwa ya kuondokewa na kiongozi wao, hivyo si uungwana kwa wengine kuendelea na sherehe katika kipindi cha maombolezo.
 

“Rais Samia Suluhu ametangaza siku 21 za maombolezo nitoe agizo katika siku hizo hakuna sherehe yoyote itakayofanyika.

“Sisi ni waungwana tuheshimu mila na desturi zetu za watanzania huu ni msiba mkubwa hatuwezi kuwa na sherehe zikiendelea.”

Mkuu huyo wa mkoa ameelekeza vyombo vya usafiri Dar es Salaam kupeleka wananchi katika uwanja wa Uhuru ambako itafanyika shughuli ya kuaga mwili wa Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021.

“Ninatoa kibali kwa vyombo vyote vya usafiri kupeleka abiria uwanja wa Uhuru bila kujali njia walizosajiliwa. Kibali hiki ni cha siku mbili Machi 20 na 21, 2021,” amesema

Amewaomba viongozi wa taasisi za Serikali, mashirika ya umma na mashirika binafsi kuwaruhusu wafanyakazi wao kwenda kutoa heshima za mwisho katika uwanja huo.