Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma, Ikulu jijini Dar es Salaam kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mama Samia alikuwa Makamu wa Rais wa kwanza Mwanamke Tanzania na wa pili kwa Afrika Mashariki. Anakuwa Rais wa tatu mwanamke Afrika waliopitia mchakato wa kidemokrasia na wa kwanza kwa Afrika Mashariki.

Hafla ya kuapishwa kwa Samia Suluhu Hassan imefanyika Ikulu jijini Dr es salaam na kuhudhuriwa na viongozi na wageni mbalimbali.

Miongoni mwa viongozi hao ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Mwinyi, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Rais Mstaafu wa awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa awamu ya awamu ya Nne Jakaya Kikwete na Aman Abeid Karume ambaye ni Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni miongoni mwa wageni waliohudhuria hafla hiyo.

Mwaka 2015, Rais Dkt John Pombe Magufuli alimchagua Samia Suluhu Hassan kuwa Mgombea Mwenza katika uchaguzi mkuu mwaka 2015 na baada ya uchaguzi huo aliapishwa kushika Wadhifa wa Makamu wa Rais.

Historia hiyo ikajirudia tena Oktoba mwaka 2020 baada ya wawili hao kushinda uchaguzi Mkuu na kushika nafasi hiyo kwa muhula wa pili.

Samia Suluhu Hassan amekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kifo cha Dkt John Magufuli Machi 17 mwaka huu.