Rais Samia Suluhu Hassan amewahakishia Watanzania kuwa yuko tayari kuliongoza Taifa kwa uwezo mkubwa alionao.

Amesema licha ya kuwa mwanamke, anatumaini kuwa ataendelea na kasi ile ile aliyokuwa nayo Dkt. John Magufuli, hivyo Wananchi hawana sababu ya kuogopa kuwa Taifa linaongozwa na mwanamke, bali watambue aliyesimama mbele yao ni Rais.

Akihutubia wakati wa shughuli ya kitaifa ya kuaga mwili wa Dkt. Magufuli katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Rais Samia amesema ameshuhudia upendo mkubwa na shukrani walizonazo Watanzania kwa aliyekuwa Rais wa Tanzania Dkt. Magufuli.

Amesema matokeo ya kazi ya uongozi wa Dkt. Magufuli yamejidhihirisha kwa hisia za Watanzania, waliojitokeza kwa wingi kumuaga katika sehemu zote mwili wake ulipopitishwa.

Rais Samia amesema alishuhudia kazi za Dkt Magufuli tangu alivyokuwa Waziri, na kwamba kiongozi huyo hakuogopa kutetea kile alichokiamini hata kama kingeweza kuhatarisha kazi yake.

Amesema yeye na viongozi wenzake wako tayari kuendeleza miradi yote iliyoanzishwa na Serikali chini ya uongozi wa Dkt. Magufuli kwa kasi ile ile aliyokuwa nayo kiongozi huyo.