Rais wa Tanzania,  Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuwa wavumilivu katika kipindi cha maombolezo ya kifo cha Dk John Magufuli na kuwahakikisha kuwa nchi iko imara.

Amesema viongozi wamejipanga  vizuri kuhakikisha wanaendelea  pale Magufuli alipoishia.

Ameeleza hayo leo Ijumaa Machi 19, 2021 mara baada ya kuapishwa kuwa kiongozi mkuu wa nchi Ikulu jijini Dar es Salaam.

“Tunayo  katiba ambayo nimeapa kuilinda na kuisimamia ambayo imebainisha vizuri hatua za kufuata pale inapotokea tukio kama hili la kumpoteza kiongozi aliye madarakani.”

“Niwaombe watanzania tuwe na moyo wa subira, tujenge umoja na mshikamano katika kipindi hiki kigumu ila nawahakikishia tuko imara,” amesema.

Amesema huu  ni wakati wa kuzika tofauti zilizopo  na kuwa wamoja kama Taifa kuhakikisha nchi inasonga mbele.

“Ni wakati wa kufarijiana  kuonyeshana upendo, udugu wetu, kudumisha utu, uzalendo na utanzania wetu. Huu si wakati wa kutazama mbele kwa mashaka bali ni wakati wa kutazama mbele kwa matumaini na kujiamini,” amesema akisisitiza kuwa si wakati wa kutazama yaliyopita bali ni wakati wa kutazama yajayo.

“Si wakati wa kunyoosheana vidole bali ni wakati wa kushikana mikono na kusonga mbele. Ni  wakati wa kufarijiana na kufutana machozi tuweke nguvu zetu kwa pamoja kujenga Tanzania yetu kama alivyotamani Magufuli,” amesema.

Akimzungumzia mtangulizi wake amesema, “Magufuli alikuwa kiongozi asiyechoka kufundisha kwa vitendo ni namna gani anataka nchi iwe. Amenifundisha mengi naweza kusema tumepoteza kiongozi shupavu, mchapakazi, mzalendo, mpenda maendeleo na mwana mapinduzi wa kweli.”