Muungano wa jeshi unaoongozwa na Marekani nchini Iraq pamoja na jeshi la nchini hiyo, umesema kuwa takriban roketi 10 leo zimeilenga kituo cha kijeshi magharibi mwa nchi hiyo kinayovihifadhi vikosi vya jeshi la muungano huo. 

Msemaji wa muungano huo wa kijeshi Kanali Wayne Marotto, amesema kuwa roketi hizo ziliilenga kambi ya jeshi la angani ya Ain al-Asad katika mkoa wa Anbar. 

Baadaye jeshi la Iraq lilitoa taarifa ya kusema kuwa shambulio hilo halikusababisha hasara kubwa na kwamba maafisa wa ulinzi walipata kifaa kilichotumika kurusha makombora hayo. 

Hili ni shambulizi la kwanza tangu Marekani ilipoilenga kambi ya jeshi la Iran katika mpaka kati ya Iraq na Syria wiki iliyopita na kuzua hofu ya kurejelewa kwa mashambulizi kadhaa ya kulipiza kisasi yalioongezeka mwaka jana na kuhitimishwa na shambulizi lililoagizwa na Marekani lililosababisha kifo cha jenerali wa Iran, Qassim Soleiman nje ya uwanja wa ndege wa Baghdad.