Rais wa Botswana,  Mokgweetsi Masisi amesema  aliyekuwa Rais wa Tanzania,  John Magufuli ataendelea kukumbukwa kwa michango wake katika kuiunganisha  Afrika.

Ameeleza hayo leo Jumatatu Machi 22, 2021 katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma inakofanyika ibada ya kitaifa ya kumuaga kiongozi huyo aliyefariki dunia Machi 17, 2021.

Amesema kiongozi huyo alikuwa na haiba ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye alipendwa na watu wengi duniani hivyo Tanzania imeendelea kuondokewa na watu muhimu.

"Kwa kumuenzi hata sisi Botswana tumeanza kufundisha Kiswahili katika shule zetu kutokana na msimamo na msisitizo wake kwa lugha hiyo, hakika alikuwa mtu muhimu sana," amesema Masisi.

Kiongozi huyo amemtaka Rais Samia Suluhu Hassan kusimama imara bila kuogopa na Watanzania wamuunge mkono ili kuyaendeleza na kuyaenzi aliyoanzisha mtangulizi wake.

Amesema Bara la Afrika limempoteza mtu muhimu aliyekuwa bado mchango wake unahitajika kwa wakati huu katika masuala ya kiuchumi.

Amesisitiza kuwa Botswana itaendelea kuwa na ushirikiano wa karibu na Tanzania kwa mambo mengi kutokana na mazuri aliyoanzisha na ndoto za Magufuli.